Jumapili, 31 Mei 2015

Mjumbe wa kamati kuu CCM, Mh.Stephen Masato Wasira atangaza nia ya kugombea urais wa Tanzania

Mwanasiasa mkongwe na mjumbe wa kamati kuu ya chama cha mapinduzi– CCM, Mh.Stephen Masato Wasira ametangaza rasmi nia ya kugombea nafasi ya rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, huku akisema kwamba ikulu haipaswi kuongozwa na rais mwenye harufu ya rushwa na ufisadi kwa madai kuwa kiongozi wa aina hiyo anaweza kuiuza nchi.
Mh.Stephen Wasira ambaye ni mbunge wa jimbo la Bunda na waziri wa kilimo, chakula na ushirika akiwahutubia wananchi katika ukumbi wa chuo cha benki kuu jijini Mwanza, amesema iwapo chama chake kitamteua kupeperusha bendera katika kinyang’anyiro cha urais na wananchi wakampa ridhaa ya kuwa rais wa awamu ya tano, atahakikisha utawala wake unakabiliana na ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, wizi wa mali na raslimali za umma.
 
Aidha Mh.Wasira ambaye amewahi kuhudumu katika wizara mbalimbali za serikali za awamu zote, amesema iwapo atapata ridhaa ya kuongoza serikali, atahakikisha kilimo cha jembe la mkono kinabakia kuwa historia kwa kutoa kipaumbele cha juu katika mapinduzi ya kilimo kwa kuzingatia kuwa asilimia kati ya 70 hadi 75 ya watanzania wanaishi vijijini na kuendesha maisha yao kutokana na kilimo na uchumi wa vijijini.
 
Kuhusu ajira kwa vijana, Mh. Wasira amesema kuwa takwimu za wizara ya kazi na ajira zinaonyesha kuwa karibu vijana milioni moja wanaingia katika soko la ajira nchini kila mwaka, lakini ni vijana laki mbili tu ndio wanaoajirwa jambo ambalo amsema uwiano huo unaweza kusaabisha matatizo ya kijamii na kisiasa kama hautashughulikiwa.