Jumatatu, 17 Agosti 2015

MISS TANZANIA IPO YATOKA KWENYE KIFUNGO



Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA) limelifungulia shindano la urembo la Miss Tanzania
baada ya mwandaaji wake Kampuni ya LINO International Agency Limited kufuata
taratibu, kuomba radhi na kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza na
kutekeleza masharti aliyopewa.





Itakumbukwa
kuwa mnano tarehe 22/12/2014 BASATA liliwaandikia barua LINO International
Agency Limited ya kulisimamisha shindano la Miss Tanzania kwa miaka miwili
(Mwaka 2015 na 2016) na kuwaagiza kujipanga upya na kurekebisha kasoro ambazo
zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.





Mapungufu
yaliyobainishwa ni pamoja na; mosi, kutokufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za
uendeshaji matukio ya Sanaa nchini, pili kutokuwasilisha nyaraka mbalimbali za
shindano lake hususan mikataba ya washiriki. Tatu kutumia mawakala
wasiosajiliwa na kupewa vibali vya BASATA.





Miongoni
mjwa mapungufu ambayo Kampuni ya LINO imeyafanyia kazi ni kuanza mchakato wa
usajili wa mawakala – BASATA na kufanyia marekebisho kanuni na taratibu za
uendeshaji wa Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania. Aidha, LINO imewasilisha
muundo wa kamati ya uendeshaji wa shindano yenye muelekeo wa kuzingatia jinsia.





Katika
kuboresha na kurudisha hadhi ya shindano la Miss Tanzania, LINO International
Agency Limited imepewa kibali cha muda kisichozidi miezi minne (4) kwa ajili ya
maandalizi ya awali ikiwemo kukamilisha usajili wa mawakala katika ngazi zote
husika.





BASATA
linapenda kuwafahamisha wadau wote wa Sanaa hususan wale wa shindano la urembo
la Miss Tanzania kwamba Kampuni ya LINO imetekeleza maagizo ya msingi iliyopewa
kama masharti ya kufunguliwa. Na kwamba baada ya kufanyia kazi changamoto
zilizokuwa zimejitokeza BASATA limeyafungulia mashindano ya Miss Tanzania kwa
masharti ya kukamilisha changamoto zilizobakia.





Ni matarajio
ya BASATA kwamba kampuni ya LINO itazingatia taratibu zote za uendeshaji wa
matukio ya Sanaa nchini na kwamba haitarudia tena makosa yatakayopelekea
kuliweka shindano hili katika hali ya kushuka hadhi na kuzua sintofahamu katika
jamii.


Sanaa ni
kazi, tuipende na kuithamini





Godfrey
Mngereza


KATIBU MTENDAJI