Release No. 146
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Septemba 7,
2014
MKATABA WA YANGA, OKWI HAUPO
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana leo (Septemba 7 mwaka huu) na kupitia
masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa kimkataba kati ya klabu ya Yanga na
mchezaji Emmanuel Okwi.
Mkataba huo ulipitiwa na Kamati ikiwemo kumsikiliza
mchezaji mwenyewe pamoja na upande wa Yanga, na kuridhika kuwa mkataba kati ya
pande hizo umevunjika.
Ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka
kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili.
Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha
kimkataba hadi kufikia Juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba
huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na
timu yoyote.
Mkataba ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa
(Okwi), ambapo Kamati imebaini kuwa uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira
ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi pamoja.
Pamoja na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa
wajumbe katika kikao kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests),
walifahamishwa kuwa kilichopo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya
Yanga na Okwi, na si usajili.
Pia lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi
Degla ya Misri. Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala
hilo na kulitolea taarifa katika kikao kijacho.
Hata hivyo mjumbe huyo hakushiriki katika kuchangia hoja
na kutoa maamuzi. Uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo
hakukuwa na suala la kupiga kura.
Kuhusu pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati
imebaini kuwa klabu hiyo imevunja mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa
kumlipa mchezaji huyo mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.
Klabu ya Coastal Union iliwakilishwa na mmoja wa
viongozi wake, wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake.
Vilevile Kamati imekubaliana na pingamizi la Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) kuhusu wachezaji waliofanyiwa uhamisho
kutoka katika mkoa wake bila kulipiwa ada za usajili, hivyo klabu husika
zinatakiwa kulipa ada hizo.
Pia Kamati imeagiza klabu zote zilizosajili wachezaji
bila kuwafanyia uhamisho, kulipa ada za uhamisho kwa pande husika kabla ya
kuanza ligi, vinginevyo leseni zao zitazuiwa hadi watakapolipa.
Mashauri mengine ya pingamizi yatasikilizwa baadaye kwa
vile klabu husika hazikupata fursa ya kufika mbele ya kamati.
Kamati inasisitiza kwa wanachama wa TFF kuheshimu
mikataba.
BONIFACE WAMBURA
KAIMU KATIBU MKUU
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)