Jumamosi, 27 Juni 2015

Mwekezaji hatarini kupokonywa shamba lenye mgogoro mkoani rukwa.


Mgogoro baina ya mwekezaji na mmiliki wa shamba la mifugo la Malonje na vijiji tisa vya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, vinavyolizunguka shamba hilo uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi sasa, umechukua sura mpya kufuatia serikali kutoa notisi ya siku tisini, inayoonesha kusudio la kutaka kusitisha umiliki wa shamba hilo kwa mwekezaji, ili hatimaye ligawiwe kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Naibu waziri wa ardhi mheshimiwa Angella Kairuki akiongea mjini Sumbawanga wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Rukwa, amesema kufuatia mgogoro huo wa muda mrefu na ulioleta madhara makubwa mkoani humo, wizara ya ardhi imeshachukua hatua za kukutana na mwekezaji, na kwamba tayari serikali kupitia halmashauri ya manispaa ya sumbawanga imeshatoa notisi hiyo ya siku tisini, ya kusudio la kufuta hati miliki ya shamba hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 15,000.

Akitoa taarifa ya utendaji wa baraza la ardhi la wilaya ya sumbawanga, mwenyekiti wa baraza hilo Bi.Frida Chinuku, amesema licha ya kufanikiwa kutatua migogoro mingi ya ardhi mkoani rukwa, lakini baraza hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na watumishi wa kutosha.