NAULI
ya Sh 1,200 iliyopendekezwa na watoaji wa huduma ya usafiri wa mabasi
yaendayo haraka (UDA RT) imepingwa na wadau wa sekta ya usafiri, badala
yake wameshauri iwe kati ya Sh 400 na 500 kutimiza malengo ya kusaidia
wananchi wa kipato cha kawaida.
Wamehoji
sababu za mabasi hayo yanayobeba watu wengi kwa safari moja na
yanayotumia barabara zisizo na foleni, yatoze nauli kubwa wakati
daladala zinazochukua abiria wachache na kukabiliwa na msongamano mkubwa
katika barabara za kawaida, wanatoza nauli za chini.
Katika
mkutano wa kupokea maoni ya wadau ulioitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa
Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kuhusu mapendekezo ya nauli
hizo, wananchi pamoja na Baraza la Walaji la Sumatra (Sumatra CCC),
walisema ukokotoaji wa UDA RT hauna weledi bali unaolenga kujipatia
faida kubwa kwa kipindi kifupi.
Wadau
hao walionya kuwa iwapo Sumatra itaruhusu mapendekezo hayo ya nauli,
wako tayari kuandamana na hata kulala barabarani kuonesha kupinga
walichoita unyonyaji unataorajiwa kufanywa na waendeshaji wa mradi huo.
Katika
mapendekezo yao, UDA RT ambao ndio watoaji wa huduma ya usafiri
wamependekeza nauli ya mtu mzima kutoka Kimara hadi Kivukoni iwe Sh 1200
na mwanafunzi alipe Sh 600.
Pia
nauli ya mabasi hayo kutoka Mbezi hadi Kimara imependekezwa iwe Sh 700
na katika njia mlisho na Sh 1,400 kwa wasafiri watakaotumia njia kuu na
njia mlisho kwa wakati mmoja.
Wanaopinga nauli
Katibu wa Baraza la Walaji la Sumatra Dk Oscar Kikoyo alisema maombi ya UDA RT hayana weledi wa kutosha.
Alisema uwekezaji uliofanywa kwenye miundombinu ya mabasi hayo nauli zinatakiwa kupungua kuliko inayotozwa na daladala.
Alisema
mabasi hayo yaendayo haraka yanapaswa kutoza nauli ya Sh 400 kwa kile
alichosema kuwa takwimu walizotoa kuhalalisha kiwango cha Sh 1,200 ni za
uongo licha ya kutoa visingizio vya ujazo wa abiria, idadi ya
watumishi, gharama za matengenezo na mishahara ya watumishi kwenye
mabasi hayo.
Alisema
katika uhalisia nauli za mabasi hayo zinatakiwa kuwa chini ya zile
zinazotozwa na daladala. Dk Kikoyo alisema haiwezekani mtu anayetoka
Posta hadi Magomeni alipe nauli sawa na anayekwenda Kimara. Alipendekeza
nauli za mabasi hayo zipangwe kwa kutegemea umbali.
“Duniani
kote nauli zinapangwa kutokana na umbali anakoenda mtu, sasa hawa
wanakuja na flat rate (kiwango sawa) haiwezekani huu ni unyonyaji,” alisema.
Aidha,
Dk Kikoyo alishauri Sumatra iache kuyapangia nauli mabasi hayo badala
yake waache nguvu ya soko iamue na washindane na daladala.
“Kibaya chajitembeza na kizuri chajiuza, Sumatra waachwe na kazi ya kusimamia usawa wa ushindani wa kibiashara,” alisema.
Alisisitiza
kuwa nauli katika sekta ya usafiri ni suala la kiuchumi ambalo
ukokotoaji wake lazima uzingatie maadili ya biashara katika soko.
Alisema DART RT hawazingatii dhana hiyo kwa makusudi ya kupata faida kubwa kwa muda mfupi.
Mwenyekiti
wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua) Hassan Mchanjama
alihadharisha kuwa iwapo Serikali itaruhusu nauli hizo, hata daladala
nyingine zitapandisha nauli nchi nzima.
Alisema
haiwezekani gari zisizokaa katika foleni zitoze nauli kubwa na gari
zinazokaa katika foleni nauli ziwe ndogo .“Hiyo haiwezekani.”
Alisema
kwa viwango vilivyowekwa abiria atajikuta anatumia Sh 5,000 kwa siku
kwa sababu atalazimika kupanda magari mengi hadi kufika mjini hali
itakayosababisha abiria kushindwa kutumia haki yao ya kusafiri.
Alisema magari yaendayo haraka yanasamehewa kodi na lengo ni mlaji apate unafuu. “Hizi gharama kubwa ni za nini sasa?,” alisema Mchanjama.
Aliongeza kuwa mabasi ya UDA RT yanabeba watu wengi hivyo watapata faida kubwa zaidi ya daladala zilizopo.
“Iweje
yatoze nauli kubwa kuliko daladala,” alihoji. Pia alisema miundombinu
ya magari hayo imejengwa kwa kodi za wananchi hivyo si busara kuwatoza
nauli kubwa wananchi kwa hali hiyo ni sawa na kumnyonya au kumkandamiza.
Watishia kuandamana
Baadhi
ya wananchi wa kawaida waliofika kwenye mkutano huo, walisema iwapo
Sumatra itaruhusu kutumika kwa nauli hizo, watahamasishana kwenda kulala
kwenye barabara za hayo magari kama ishara ya kuzipinga.
Nao
waliomba nauli iwe kama ya daladala za kawaida. Azim Dewji alisema
nauli iwe kati ya Sh 500 na 600 kwa maelezo kuwa hiyo nauli ya Sh 1,200
italeta mvurugano kwenye jamii.
“Nendeni mkakae tena mtafakari nauli hii, mmeona ilivyoleta tafrani humu ukumbini.” Mjengi
Gwao ambaye ni mwasisi wa mradi huo, naye alipinga nauli hizo na
kueleza kuwa mpango wa Serikali kuleta mradi huo ni kuwasaidia wananchi
masikini.
Alikuja mtaalamu wa Benki ya Dunia akatuambia kuwa mradi huo utawakomboa watu masikini kwani watalipa nauli ya chini.
“Nashangaa
leo tunaambiwa nauli Sh 1,200, hili si lengo la mradi, mimi nilienda
Bogota (Colombia) na ujumbe wa Serikali kujifunza juu ya mradi huu,
waendeshaji wa mabasi haya wanapotosha umma na Sumatra iwakatalie,” alisema.
Abdul
Awadhi ambaye pia ni miongoni mwa waanzilishi wa mradi huo, alisema
wataalamu kutoka Benki ya Dunia waliwasilisha andiko lao na kueleza kuwa
mradi huo ukianza nauli ziwe kati ya dola za Marekani 0.3 na 0.2 kiasi
ambacho ni Sh 400 na 500.
Alisema
hata bei za mabasi waliyopigia wakati ule ndio ambayo waendeshaji
wameiweka jana na akahoji “sasa hivi nauli kubwa zinatoka wapi?
Aidan
Eyakuze kutoka Twaweza alisema ongezeko la nauli ya Sh 700 kutoka Sh
400 ni kubwa na wananchi hawawezi kumudu kwani wananchi watakuwa
wanatumia kipato chao chote cha mwezi kwa ajili ya kulipia usafiri.
Mwingine
aliyejitambulisha kwa jina la Msafiri alisisitiza nauli iwe Sh 400 na
akasema kama Sumatra itapuuza, wako tayari kuandamana kuipinga nauli ya
Sh 1,200.
Kwa
upande wake, Steven Kahumbi alisema mtu mmoja atakuwa anatumia Sh
16,800 kwa wiki kwa ajili ya nauli jambo ambalo alisema kwa kipato cha
Watanzania kiwango hicho ni kikubwa.
Kwa nini 1,200/-?
Akiwasilisha
mada kuhusu ukokotoaji wa nauli hizo na sababu za kuweka kiwango hicho,
Mkurugenzi Mtendaji wa UDArt David Mgwassa alisema magari hayo
yatafanya safari zake kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 5 usiku na
yatakuwa na madereva wawili ambao watafanya kazi kwa kupokezana.
Alisema
basi litaondoka kituoni kila baada ya dakika tano na litaondoka hata
kama lina abiria mmoja na nyakati za usiku litandoka kila baada ya
dakika 10. Alisema abiria wa mabasi hayo watakata nauli yao kwa kutumia
mfumo wa elektroniki.
Alisema katika makadirio waliyofanya basi hilo litajaza asilimia 51 ya abiria kwa kila safari kutokana na kutosubiri abiria.
“Nauli
hizi tumeziweka kwa sababu uendeshaji wa magari haya ni tofauti na
daladala, kuna wakati magari yatalazimika kwenda tupu maana hayasubiri
abiria ila muda wake ukifika linaondoka,” alisema Mgwassa na kuongeza kuwa kwa siku kila gari litafanya safari mara 22.
Pia
alisema wameweka kiwango hicho kwa kuwa wafanyakazi wa mabasi hayo
watalipwa mishahara ya Sh 800,000 kwa mwezi na watalipiwa kodi ya PAYE,
watawekewa akiba kwenye mifuko ya pensheni na hakuna ruzuku yoyote
ambaye itawekwa na Serikali hivyo gharama zote zitabebwa na waendeshaji
wa mradi huo.