Jumapili, 24 Mei 2015

Rais Kikwete awataka viongozi wa CCM kuweka tofauti zao pembeni na kuhakikisha wanapitisha majina ya wagombea wenye sifa.

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi  Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa CCM kuweka tofauti zao pembeni na kuhakikisha wanapitisha majina ya wagombea wenye sifa na wanaokubalika na wananchi kwenye uchaguzi mkuu ujao ili kukiwezesha chama hicho kushinda kwa kishindo.
Mwenyekiti huyo anatoa angalizo hilo wakati akifungua mkutano mkuu wa halmashauri kuu ya CCM {NEC} ambapo ameonya endapo viongozi wa chama hicho watapitisha majina ya wagombea kwa utashi wao na kusahau kuwa nguvu kubwa ya ushindi iko kwa wananchi ambao ndio wengi chama hicho kisitarajie kuibuka na ushindi mkubwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
 
Awali kabla ya Rais Kikwete kufungua NEC kamati kuu CCM imefanya tathmini ya mwenendo wa mchakato zoezi la upigaji wa kura ya maoni ya katiba mpya na kuitaka serikali kujadiliana  na tume ya taifa ya uchaguzi NEC ili kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazolikabili zoezi hilo ambazo zinaweza kuwa kikwazo kwa kura hiyo kwenda sambamba na uchaguzi mkuu ujao kama ilivyotangazwa awali.
 
Kamati hiyo ambayo inalazimika kukaa kwa siku mbili mfululizo kinyume na ratiba iliyotolewa awali ya siku moja kinatoa ushauri huo baada ya kupitia hoja mbalimbali ambapo pamoja na mambo mengine imebaini zoezi la upigaji kura ya maoni ya katiba mpya linakbiliwa na changamoto lukuki zikiwemo kasi ndogo ya uandikishaji wa daftari la kudumu.
 
Changamoto zingine zilizobainishwa kuikabili kura hiyo ni pamoja na matakwa ya kisheria ambayo yanaelekeza zoezi hilo liende pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kwa siku 60 siku 30 za kampeni na baada ya hapo ndipo ipigwe kura ya maoni ambapo tathmini inaonyesha hakutakuwepo na muda wa kutosha kabla ya tarehe 25 October inayotajwa kuwa ndio tarehe rasmi ya uchaguzi mkuu.