MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia waliokuwa Mawaziri wastaafu Basil
Mramba na Daniel Yona kutumikia adhabu ya kifungo cha nje kwa kufanya
usafi katika maeneo ya kijamii ikiwemo Hospitali ya Sinza Palestina.
Hatua
hiyo inatokana na Mramba ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Yona
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, kupitia Mawakili wao kuwasilisha
barua mahakamani hapo kutoka Magereza kuhusu kutumikia kifungo cha nje.
Mawaziri
hao wa zamani waliwasilisha barua hiyo ya kuitaarifu mahakama yenye
kumbukumbu namba 151/DA/3/11/223 ya Desemba 5, mwaka jana, wakiongozwa
na jopo la mawakili wao watatu Peter Swai, Cuthbert Nyange na Elisa
Msuya.
Katika barua hiyo waliyoiwasilisha kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘Wafungwa wenye sifa ya kutumikia vifungo vyao chini ya Mpango wa Huduma kwa Jamii”.
Hakimu
Mkeha alisema mchakato huo ulianza baada ya Magereza kuwasilisha barua
hiyo mahakamani hapo kwa kupeleka majina ya watu wanaotumikia kifungo
cha nje ikiwemo mawaziri hao.
Alisema
mahakama haihusiani na mchakato huo, kwani ilishamaliza kazi yake ya
kuhumu, hivyo jukumu la kutumikia kifungo cha nje ni kazi ya Magereza.
“Baada
ya kuleta barua hiyo kisheria mahakama inaishinikiza Ustawi wa Jamii
ili ifanye uchunguzi kutokana na majina yaliyowasilishwa mahakamani,”alisema.
Hakimu
Mkeha alisema kupitia barua hiyo, Mawaziri hao wa zamani wamepangiwa
kutumikia adhabu ya kufanya usafi kwenye Hospitali ya Sinza Palestina
kwa saa nne za kila siku.
Alisema
awali kabla ya mahakama kuridhia adhabu hiyo, iliwaita Mawaziri hao kwa
ajili ya kuwahoji kama wameridhia na adhabu watakayopangiwa sambamba na
vipengele vinavyowahusu.
“Kutokana
na barua hiyo mahakama ikaona ni vyema kuwaita wahusika wenye ambapo
tuliwahoji kama wanaridhia kutumikia adhabu hiyo, ambapo walikubali
ndipo tukaridhia,”alisema.
Kuhusu
masharti yaliyotumika kuwapatia kifungo hicho, alisema kinatokana na
sheria ya Jamii namba 6 ya mwaka 2002, kifungu cha 3(1).
Alisema
baadhi ya vigezo vinavyotumika kwa wafungwa kutumikia adhabu ya nje ni
muangalio wa ripoti yao ilikuwa inasemaje, umri, washtakiwa kama
walishawai kutiwa hatiani, makosa namna yalivyo, kama wanafamilia, pia
kama wanakubali kuitumikia jamii, kama wana ajira, tabia za mshtakiwa na
umbali wa eneo analokaa na anapofanyia adhabu hiyo.
Inakumbukwa
kuwa Oktoba 2, 2015 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa
hukumu ya rufaa dhidi ya mawaziri wastaafu, Basil Mramba na Daniel Yona
ambapo Jaji Projest Rugazia, alikubaliana na hoja kwamba kwa mujibu wa
mashtaka yaliyowatia hatiani kwa matumizi mabaya ya Ofisi na kwa mujibu
wa kifungo cha 35 cha adhabu PC ambacho Mahakama ilikitumia walipaswa
kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili na si miaka mitatu.
Katika
rufani hizo, Mramba na Yona, waliwasilisha hoja tano kupinga hukumu
iliyotolewa Julai 6, mwaka jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
na jopo la Mahakimu watatu, likiongozwa na John Utamwa.
Aidha
DPP alipinga adhabu waliyopewa mawaziri hao kwa madai ni ndogo, pia
hakimu alikosea kumuachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,
Gray Mgonja na pia iliiomba mahakama iamuru washtakiwa walipe fidia ya
fedha walizosababisha hasara.
Katika uamuzi huo Jaji Rugazia alikubali hoja ya kina Mramba kuwa walipewa adhabu mbili kwa kosa moja.
“Haikuwa
sahihi kuwashitaki kwa kosa la kusababisha hasara wakati kosa hilo
lilishakuwa kwenye makosa mengine ambayo ni la tano hadi la 10,” alisema.
Aidha,
alisema Yona aliunganishwa kimakosa katika shtaka hilo, hivyo alifuta
shitaka hilo pamoja na adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini
ya Sh milioni tano iliyotokana na kosa hilo.
“Ninaondoa
shitaka la kusababisha hasara, ninafuta adhabu ya kifungo cha miaka
mitatu jela na faini ya Sh milioni tano, hivyo Yona na Mramba
watatumikia kifungo cha miaka miwili kwa kila kosa,“ alisema.
Katika uamuzi huo, Jaji Rugazia alisema,
“Nakubali Kifungu cha 6 cha Kanuni ya Adhabu kinachotaka mahakama itoe
amri washitakiwa walipe fidia, lakini siwezi kutoa amri hiyo.”
Pia
alikataa hoja za kina Mramba kuwa hati ya mashtaka ni batili, pia
alisema hakukuwa na njama zozote kwa upande wa Jamhuri kutoita mashahidi
waliosaini mkataba huo ili kuathiri upatikanaji wa haki, kwa kuwa
utetezi walikuwa na haki ya kuomba watu hao wawe mashahidi wao.
Alisema
wasitumie maelezo ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa,
kuficha kosa kwa kuwa alitoa maelekezo kutokana na barua aliyoipata
kutoka kwa Mramba na hakujua kama tayari Mamlaka ya Mapato nchini (TRA)
ilishatoa angalizo la kutokutoa msamaha huo.
Kwa
upande wa Mgonja, Jaji Rugazia alisema anahalalisha kuachiwa kwake huru
baada ya kutopatikana na hatia. Alisema, “Siwezi kuilaumu mahakama kwa
kumuachia huru”.
Katika
hukumu hiyo, mawaziri hao walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na
kulipa faini ya Sh milioni tano, baada ya kupatikana na hatia ya
matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh
bilioni 11.7.
Kwa
mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani mwaka 2008,
wakikabiliwa na mashtaka ya kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho
cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua
madini ya dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.