Serikali
imebaini wizi wa takribani shilingi Milioni 700 katika Shirika la
Ndege Tanzania (ATCL) kupitia kampuni ya Wakala wa ukatishaji tiketi ya
Salama World Travel iliyopo visiwa vya Komoro.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ,Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa ameeleza kuwa wizi
huo umefanywa kwa kushirikiana na wafanyakazi wa shirika hilo.
“Kufuatia
upotevu huo Serikali imechukua hatua thabiti ikiwemo kumsimamisha kazi
Mkurugenzi wa Fedha wa ATCL Bw.Steven Kasubi ili kupisha uchunguzi
utakaofanywa na kikosi cha polisi kitengo cha usalama mtandaoni ili
kubaini mtandao mzima uliohusika ” alisema Prof.Mbarawa.
Aidha
aliongeza kuwa kwa utaratibu wa kawaida wa shirika hilo wakala anapewa
ruhusa ya kuuza tiketi za ndege kuanzia kiasi cha shilingi milioni 15
tu na pale anapomaliza mauzo anarudisha fedha kwa shirika na baadaye
kupewa ruhusa tena.
Prof.Mbarawa
anasema kwa sasa wameanza na shirika la Ndege la Tanzania kwa kwa lengo
la kulifufua kwa kununua ndege mpya na kuwa na wafanyakazi wachapakazi
na waadilifu.
“Siku
mbili zilizopita nilifanikiwa kukutana na menejimenti ya ATCL na
kubaini mapungufu mengi na hivyo kuamua kuyafanyia kazi kwa kuhakikisha
shirika hii linarudi kutenda kazi kwa udhabiti kwa kuwashughuikia wale
wote wanaoenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma” alisema Prof.Mbarawa.
Vilevile
aliongeza kuwa Serikali imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali(CAG) kufanya uchunguzi kwa mawakala wengine wote wa Shirika
hilo kubaini kama fedha za uuzaji wa tiketi hizo zinarudishwa kama
inavyotakiwa.
Prof.Mbarawa
ametoa wito kwa wananchi kuachana na wizi kwa njia ya mtandao kwa kuwa
sheria ya mtandao iliyoanzishwa mwaka jana inatumika katika kuhakikisha
kuwa watuhumiwa wanafikishwa katika mkondo wa sheria na kuchukuliwa
hatua stahiki.