Jumatatu, 25 Mei 2015

NEC yatoa ratiba ya uchukuaji fomu ndani ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu.


Hatimaye kitendawili cha kuanza kwa michakato ya uchukuaji fomu za kuwania uongozi wa dola ndani ya chama cha mapinduzi {CCM} kuelekea uchaguzi mkuu ujao kimeteguliwa baada ya kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho NEC kutoa ratiba huku nafasi ya urais wa jamuhuri ya muungano wagombea wakitakiwa kuchukua fomu kuanzia June tatu mpaka Jully mbili mwaka huu.
Akitoa ratiba hiyo katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Nape Nnauye amesema wagombea urais wa jamuhuri ya muungano na ule wa Zanzibar watatakiwa kuchukua fomu kuanzia tarehe tatu june na kuzirudisha tarehe 2 jully na katika kipindi hicho pamoja na mambo mengine watatakiwa kutafuta wadhamini wasipopungua 450 kwa nafasi ya jamuhuri kutoka mikoa 15 mitatu kati yake iwe Zanzibar na urais wa Zanzibar wadhamini 250 kutoka mikoa mitatu ya Zanzibar.
 
Mara baada ya zoezi hilo litafuatiwa na vikao mbalimbali vya uchujaji wa majina ya wagombea kwa kuanza na kikao cha kamati ya usalama na maadili tarehe 8/7 kikifuatiwa na kikao cha kamati kuu tarehe 9/7 halafu halmashauri kuu ya CCM NEC itakayotoa jina la mgombea wa urais tarehe 10/7na kisha mkutano mkuu utakaofanyika tarehe 12/13 mwezi jully.
Kwa upande wa nafasi za ubunge na udiwani na baraza la wawakilishi wagombea watatakiwa kuchukua fomu kuanzia tarehe 15-19 mwezi jully ambapo kampeni za ushawishi kwa wanachama kwenye matawi zitafanyika kuanzia tarehe 20 mpaka 31 jully ambapo kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea katika ngazi hizo zitapigwa sambamaba tarehe 1/08 2015 huku wagombea wote wakitakiwa kuzingatia maelekezo ya kanuni na taratibu za chama hicho.