Rais
John Magufuli amewataka watendaji wote wa serikali kuhakikisha kuwa
wanatekeleza ipasavyo matakwa ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa
ndicho kinachoongoza nchi kwa sasa.
Magufuli
ametoa agizo hilo leo kwenye sherehe za miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama
cha Mapinduzi zilizofanyika katika uwanja wa Namfua mjini Singida.
Rais
Magufuli ambaye alikuwa ni miongoni viongozi wakuu wa serikali
waliohudhuria sherehe hizo akiambatana na makamu wake Samiah Suluhu
Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema yeye na serikali yake
wamejipanga kutekeleza kikamilifu ilani ya CCM na kwamba hawezi
kukiangusha chama hicho.
Akitoa
salam zake katika sherehe hizo, Magufuli ametumia muda usiozidi dakika
10 kueleza mambo ambayo tayari serikali yake imeanza kuyafanya na ambayo
itaendelea kuyafanya ikiwa ni pamoja na "kutumbua majipu" kwa ustawi wa
maisha ya watanzania wote bila kujali vyama vyao.
Ametumia
nafasi hiyo kuwaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya pamoja na
watendaji wote serikalini kufanya kazi kwa nguvu, uadilifu na uzalendo
ili kuwaletea watanzania maendeleo, na kwamba atakayeona hawezi
atamuweka pembeni ili wengine wafanye kazi.
“Nawaeleza
watendaji wote serikalini kuwa atakayeshindwa kufanya kazi, nitamueleza
kwa upole sana maana mimi ni mtu mpole, nitamuambia akae pembeni apishe
wengine”
Rais
Magufuli pia ameupongeza uongozi wa CCM mkoa wa Singida kwa kuchangia
madawati 1000 kwa shule za Singida na kuwaagiza wakuu wote wa mikoa na
wilaya kuhakikisha wanafunzi hawakai chini.
“Mh
mwenyekiti inasikitisha sana kuona sisi tunajifungia kwenye maofisi
makubwa yenye viyoyozi, na maviti ya kuzunguka lakini tukitoka tu nje
tunakuta wanafunzi wamekaa chini kwenye mavumbi, sasa nawaagiza wakuu wa
wilaya na wakuu wa mikoa hakikisheni wanafunzi hawakai chini”
Rais
Magufuli pia ametumia nafasi hiyo kukishukuru Chama cha Mapinduzi
kufanikisha yeye kuwa Rais kwa kuwa bila chama hicho yeye asingekuwa
Rais.
“Nataka
watanzania wote wajue kuwa bila CCM mimi nisingekuwa Rais wao, kwa hiyo
huwezi kunitenganisha mimi na CCM, ndiyo maana leo nimekuja nimevaa
kijani yangu hapa”
Pia amesema haoni kama kuna chama kingine chochote kitakachokuja kutawala Tanzania zaidi ya CCM
"Nataka
ifikie hatua watanzanie wote wasiwaze wala kuota vyama vingine,
tutafanya yale ambayo wao wanataka kuyafanya, ... Hakuna mtawala
anayetaka kutawaliwa, tena kwa bahati mbaya atawaliwe na vyama vya
hovyohovyo, CCM itaendelea kutawala"