Mchezo wa ligi kuu ya Soka Tanzania bara kati ya City na Tanzania Prison uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine ukimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Kwenye mchezo huo uliokuwa wa kasi muda wote timu zote zilifanya mashambulizi ya mara kwa mara kwenye lango la mwenzake huku City ikipoteza nafasi ya wazi katika dakika ya 10 baada mpira uliopigwa na Temi Felix kutoka nje kidogo ya lango la Prison na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya 30, Ditram Nchimbi alishindwa kuiandikia City bao baada kuunganisha vibaya mpira uliopigwa na Ramadhan Chombo na kuwa kona ambayo iliokolewa na walinzi wa Tanzania Prisons, hivyo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo yalibaki kuwa 0-0.
Kipindi cha pili kocha Mohamed Kijuso alifanya mabadiliko kwa kumtoa Deo Julius aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na John Jerome na baadae kumtoa Temi Felix na kuingia Haruna Moshi ambaye alifanikiwa vizuri kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji .
Haruna Moshi nusura aipatie City bao kwenye dakika ya 75 baada ya kuunganisha vizuri mpira wa Ditram Nchimbi kutoka upande wa kushoto hata hivyo uimara wa kipa wa prison, uliisaidia timu yake kuepuka kufungwa baada ya kupangua mpira huo na kuwa kona mabayo haikuzaa matunda, hivyo hadi dakika 90 zinakamilia City 0 Prison 0
Mara baada ya mchezo kocha msaidizi Mohamed Kijuso alisema, mchezo ulikuwa mgumu ambao ungeweza kuleta matokeo yasiyotarajiwa lakini anashukuru kupatikana kwa pointi moja ambayo itakuwa chachu kuelekea mchezo Kwa upande wa Mayanga yeye alisema vijana wake walicheza chini ya kiwango tofauti na michezo mingine wanajipanga na mchezo ujao watayafanyia malekebisho makosa madogo waliyoyafanya.