Waziri
wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mwigulu Nchemba amewasimamisha kazi
viongozi wa vyama vya msingi vya tumbaku mkoani Iringa wanaotuhumiwa
kushiriki katika ufisadi wa mkopo wa matrekta 9 kupitia mgongo wa vyama
vya msingi vya wakulima wa tumbaku na kujimilikisha wenyewe.
Matrekta hayo 9 yaliyoleta mzozo vilikopeshwa vyama vya Msingi na benki ya CRDB kwa manufaa ya wote na wakulima wamekuwa wakitozwa pesa wanapoyatumia matrekta hayo ili kulipia madeni benki.
Katika utetezi wao, viongozi hao wa vyama walimwambia Waziri kuwa Matrekta hayo siyo ya vyama bali ni ya kwao ila walikopa kupitia mgongo wa Vyama vya msingi vya ushirika.
Waziri Nchemba aliwahoji viongozi hao kama kuna kiongozi aliyelipia mkopo wa matrekta hayo kwa fedha yake ambapo wote walisema hawajalipia ila wamelipiwa na wanachama lakini walipanga yatakuwa ya kwao kwa kuwa wao ndio wanaosimamia ukusanyaji wa fedha za wanachama kuyalipia Matrekta hayo.
Utetezi huo ulimtia kichefuchefu Waziri Nchemba na kuamua kuwafukuza kazi viongozi hao na kuamuru benki ya CRDB waandike kadi za matrekta hayo kwa umiliki wa vyama vya Msingi.