Mama mzazi wa kocha mkuu wa Mbeya City Fc, Juma Mwambusi, Bi Stumai Jafari (72) amefariki dunia alfajiri ya kuamkia leo akiwa njiani kurejeshwa jijini Mbeya baada ya matibabu ya siku kadhaa kwenye hospital ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na akiongea na harubutz, Omary Mwambusi ambaye ni mdogo wake kocha Juma Mwambusi, alisema kuwa Marehemu mama yake amekuwa akisumbuliwa na matatizo mbalimbali kiafya ambayo kwa namna moja ama nyingine yalikuwa yanachangiwa umri wake kuwa mkubwa (utu uzima) na pia kansa iliyokuwa inamsumbua toka mwaka jana.
“Tutafanya maziko jioni ya leo saa 10,mara baada ya taratibu zote kukamilika ikiwemo za kidini, Marehemu mama alikuwa anasumbuliwa na matatizo mbalimbali kiafya, hii ni kwa sababu ya umri mkubwa, pia Kansa iliyoanza kumsumbua toka mwaka jana, alinza matibabu hapa jijini Mbeya kwenye hospital ya Rufaa na baadae tukaamua kumhamishia jijini Dar kwenye hospital ya Muhimbili ambako amekaa kwa takribani majuma mawili” alisema
Akiendelea zaidi Omary alisema kuwa, jana jumanne waliamua kumrudisha jijini Mbeya baada ya kupata nafuu akiwa muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu, lakini wakiwa njiani Bi Stumai alifariki dunia, marehemu ameacha watoto 9 na wajukuu 27 .
Uongozi waharubutz unaungana na familia ya Marehemu katika kumuomba mungu ajaalie nguvu na moyo wa uvumilivu kwa wote walioguswa na msiba huu na pia kuomba ushirikiano wa pamoja katika kipindi hiki kigumu.inna lillahi wa inna ilaihi raj un