Wakati chama cha waandishi wa habari wanawake(TAMWA) kikilaani ukatili katika jamii mwanamke mmoja mkazi wa Sokoine Road mjini Songea mkoani Ruvuma Bi.Rehema Gwaya amefanyiwa ukatili na mke mwenzake kwa kumwagiwa mafuta ya moto usoni na kuungua sehemu mbalimbali za mwili wake.
Bi. Rehema Gwaya ambaye amelazwa katika Hospitali ya mkoa Songea akiwa na mwanae wa miezi saba anasema chanzo cha kufanyiwa ukatili huo ni kutofautiana na mke mwenzake aitwaye Zefania Chimgege baada ya kuhoji masuala ya usafi ambapo zefania aliyekuwa akipika maandazi akamwagia karai la mafuta ya moto usoni.
Baada ya kufanyiwa unyama huo shemeji yake ambaye ni mume wa Zefania Bw.Hafidhi Hamidu Mbaya akamwambia atoke nje ammalizie kwa kumchoma na kisu.
Mganga mfawidhi katika hospitali ya mkoa Songea(HOMSO) Dkt.Benedikt Ngaiza ameelezea hali ya mgonjwa huyo huku wakazi wa songea wakilaani ukatili huo.
Rehema Gwaya na Zefania Chimgege wameolewa sehemu moja na wote wanaishi katika nyumba ya baba Mkwe na waume zao na kwamba zefania chimgege anashikiliwa na polisi kwa kufanya ukatili huo.