Jumapili, 7 Juni 2015
MBEYA CITY WAMVUTIA KASI MWAMBUSI
UONGOZI wa Mbeya City umesema unaendelea kufanya mazungumzo na Kocha wao Juma Mwambusi ili kumpa mkataba mpya wa kuifundisha timu hiyo kwa msimu ujao.
Mwambusi amemaliza mkataba wake na hadi sasa hajapewa mwingine utakaompa nafasi ya kuendelea kuifundisha timu hiyo.
Akizungumza na mtandao huu Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema wana mpango wa kuendelea na Kocha huyo hivyo wanafanya mazungumzo naye na ikiwa watakubaliana wataweka wazi.
“Ni kweli Mwalimu amemaliza mkataba wake lakini bado tunaendelea na mazungumzo tunaamini mambo yatakuwa mazuri,” alisema.
Akizungumzia kuondoka kwa wachezaji wao, alisema Mbeya City haitishwi na hilo kwani watasajili wengine wenye uwezo.
Wachezaji ambao wamesajiliwa na timu nyingine ni Deus Kaseke alisajiliwa Yanga, Peter Mwalyanzi aliyesjailiwa Simba, Paul Nonga Mwadui Fc na baadhi ya wengine ambapo wote wamekwenda wakiwa huru.
City tayari imeshafanya usajili wa nyota watatu, Gideon Brown kutoka Ndanda Fc, Haruna Shamte kutoka JKT Ruvu na Joseph Mahundi aliyekuwa akicheza kwenye kikosi cha Coastal Union ya Tanga.