MKUU
mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye ni Rais mstaafu
Jakaya Kikwete, ametembelea chuo hicho kujifunza na kujionea hali halisi
ilivyo, kabla ya kukabidhiwa rasmi wadhifa huo.
Kikwete
aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, ameteuliwa hivi karibuni na Rais John
Magufuli kushika wadhifa huo, baada ya kufariki kwa Balozi Fulgence
Kazaura mwaka 2013.
Akiwa
chuoni hapo majira ya mchana, Kikwete alitembelea Chuo cha Uhandisi,
Jengo jipya la Sayansi, kumbi za mihadhara za Yombo na eneo ambalo
itajengwa maktaba mpya ya kisasa.
Akiwa
katika Ukumbi wa Yombo, aliwaambia wanafunzi kuwa Rais John Magufuli
amempa kazi ya kuwa mkuu wa chuo, hivyo amefika hapo kujionea hali
halisi kabla ya kukaa na viongozi kutengeneza chuo hicho kiwe bora
zaidi.
Akiondoka
katika eneo la ukumbi huo, baadhi ya wanafunzi walimfuata na kumweleza
kuwa zaidi ya miezi miwili hawajapewa fedha za kujikimu, hivyo
aliwaahidi kuwasaidia kwa kulisemea sehemu husika.
Baada
ya ziara hiyo, Kikwete alikutana na watendaji mbalimbali wa chuo hicho
na kuwaeleza kuwa ujio huo umempa kukifahamu chuo hicho kwa sehemu. “Nimefurahi fursa hii ya kutembea leo (jana) kabla ya siku rasmi ya kukabidhiwa uongozi wa chuo.
"Bado
natamani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiwe bora kuliko vyote nchini.
Sina maana vingine vitakuwa duni, hapana. Ila kiwe ni chuo kinachotoa
viongozi. Mtu akitaka kiongozi aanzie kumtafuta kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, akikosa ndio aende chuo kingine.
"Na hivyo vyuo vingine watafute maeneo ambayo watayakomalia ili nao wafuatwe,” alisema Kikwete ambaye alisoma hapo katika miaka ya 1970.
Alisema
amesikia kilio cha wanafunzi hao baada ya kumwambia hali ni tete kwa
kuwa hawajapata fedha, hivyo japo hajakabidhiwa rasmi nafasi hiyo,
ataanza na hilo ili vijana wasome vizuri.
Aliahidi
kurudi kabla ya mwezi huu kuisha ili akutane na viongozi mbalimbali,
lengo ni kukielewa vizuri kabla ya kukabidhiwa rasmi.