Timu ya Taifa
ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajiwa kuingia kambini kesho jumatano
katika hoteli ya Tansoma iliyopo eneo la Gerezani jijini Dar es salaam
kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri kuwania kufuzu kwa AFCON.
Kocha Mkuu wa
Taifa Stars Mart Nooij, amewaita wachezaji 16 kuingia kambini kesho siku
ya jumatano kwa ajili ya kupimwa afya zao na kujua maandeleo yao kabla
ya kuwajumisha katika kikosi cha pamoja kitakachokua kwenye maandalizi
ya mchezo dhidi ya Misri.
Wachezaji
walioitwa kuingia kambini kesho ni, Mohamed Hussein, Peter Manyika,
Hassan Isihaka, Jonas Mkude (Simba SC), Salum Telela, Juma Abdul, Nadir
Haroub (Yanga SC), Aishi Manula, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Kelvin
Friday (Azam FC), Rashid Mandawa, Atupele Green (Kagera Sugar), Haroun
Chanongo (Stand United) Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Emmanuel Simwanda
(African Lyon).
Mara baada ya
kurejea kutoka nchini Afrika Kusini, kocha wa Stars Nooij aliwapa
mapumziko ya siku 10, wachezaji waliokua kwenye michuano ya Cosafa mpaka
Juni Mosi ambapo ndipo watajumuika na wachezaji wengine waliopo
kambini.
Ifikapo Juni
Mosi, 2015 Taifa Stars itaanza kambi ya moja kwa moja kujiandaa na mechi
dhidi ya Misri itakayochezwa jijini Alexandria katika uwanja wa Borg El
Arab Juni 14, 2015 ikiwajumuisha pia wachezaji Mbwana Samatta na Thomas
Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya
Congo DR.
Kabla ya
kuelekea nchini Misri, Taifa Stars inatarajiwa kuweka kambi jijini Addis
Ababa nchini Ethiopia kuanzia tarehe 4,Juni 2015 kwa muda wa wiki moja
kabla ya kuelekea nchini Misri kwenye mchezo huo dhidi ya Mafarao.