Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limetangaza viingilio vya
mchezo kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) dhidi ya
timu ya Taifa ya Zambia (She-Polopolo) kiingilio cha juu sh.5,000 kwa VIP na
sh. 2,000 kwa majukwaa yaliobakia, mechi hiyo itachezwa ijumaa jioni saa 10 kwenye
dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Twiga Stars chini ya kocha mkuu Rogasian Kaijage imeendelea
kujifua katika hosteli za TFF zilizopo Karume, kuhakikisha inaibuka na ushindi
katika mchezo huo wa kuwnaia kufuzu kwa Michezo ya Afrika nchini Congo-
Brazzavile mwezi Septemba mwaka huu.
Katika mchezo wa awali uliofanyika wiki tatu zilizopita jijini
Lusaka nchini Zambia, Twiga Stars iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya
wenyeji Zambia, hivyo katika mchezo wa ijumaa kuhitaji ushindi wa aina yoyote
tu ili kuweza kufuzu kwa fainali hizo.
TFF inawaomba wapenzi, wadau na washabiki wa mpira wa miguu
nchini, kujitokeza kwa wingi siku ya ijumaa jioni uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam kuja kuwapa sapoti Twiga Stars watakapokuwa wanapeperusha bendera ya
Taifa.
Wakati huo huo, timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia (She-Polopolo)
inatarajiwa kuwasili usiku wa saa 7.25 kuamkia alhmisi kwa shirika la Ndege la
Ethiopia wakiwa na msafara wa wachezaji 18 na viongozi saba na watafikia katika
hoteli ya Tansoma iliyopo eneo la Gerezani Kariakoo.
Msafara wa Zambia (She-Polopolo) unaongozwa na mkuu wa msafara Lenny
Khuwa, kocha mkuu Albert Kachinga, kocha msaidizi Kape Saili, kocha wa
magolikipa Yona Phiri, daktari wa timu James Nyimbili, mchua misuli Conerlia
Chazura, na meneja wa timu ni Besa Chibwe.
Wachezaji wanaotarajiwa kuwasili ni Rachel Nachula, Annie Kibanji,
Chiko Nkhoma, Osala Kaleo, Joana Benai, Meya Banda (Nahodha), Misozi CR
Chisamu, Jane Nshika Chalwe, Milika Limwanya, Mary Wilombe, Grace Chanda,
Barbra Banda, Memory Mwaseba, Hazel Natasha Nali, Martha Tembo, Mary Mwakapila
na Ireen Lungu.
Kesho jioni She-Polopolo wanatarajiwa kufanya mazoezi katika
uwanja wa Taifa, uwanja ambao ndio utakaotumika kw amchezo huo.
Waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Uganda wanatarajiwa kuwasili
leo mchana ambao ni Ms Anna Akoyi , Ms
Nakkito Nkumbi , Ms Jane Mutonyi, na Ms
Nabikko Ssemambo, Kamishina wa mchezo Ms
Nomsa Jacobeth Mhalangu kutoka nchini Afrika Kusini anatarajiwa kuwasili leo
jioni.
TFF YAMPONGEZA TENGA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi,
amempongeza Bw Leodgar Tenga kwa kuchaguliwa kuendelea kuwa mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).
Aidha Rais Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa wajumbe waliochaguliwa kuwa wajumbe wapya wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu baranai Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Duniani FIFA.
Katika salamu hizo na nakala zake kutumwa kwa Rais wa CAF Bw. Issa
Haytou na Rais wa FIFA Bw. Blatter, Malinzi amewatakia kila la kheri katika
majukumu hayo mapya,na kwa ajili ya
maendeleo ya mpira wa miguu duniani.
Tenga amechaguliwa nafasi hiyo baada ya kuwa mgombea pekee kutoka
kanda ya Afrika Mashariki aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo na kuungwa mkono na
nchi zote wanachama wa CECAFA.
NB: Kesho alhamisi saa 5 kamili asubuhi kutakua na
mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano wa TFF uliopo Karume,
makocha wa Twiga Stars na She-Polopolo wataongelea maandalizi ya mwisho
kuelekea mchezo wa siku ya ijumaa.