Alhamisi, 3 Machi 2016

NSSF Haina Mkurugenzi wala Kaimu kwa Wiki Mbili Sasa


Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) linamaliza siku ya 15 likiwa halina kiongozi baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Dk Ramadhan Dau kuteuliwa kuwa balozi na kuacha mara moja shughuli za kila siku za taasisi hiyo kubwa, hali iliyofanya shughuli zake kudorora.

Rais John Magufuli alimteua Dk Dau kuwa balozi Februari 15, sambamba na makada wengine wawili wa CCM, Dk Asha Rose Migiro na Mathias Chikawe, akisema vituo vyao vya kazi vitajulikana baada ya taratibu za kidiplomasia kukamilika.

Tangu wakati huo, NSSF imekuwa ikijiendesha bila ya kiongozi mkuu na habari kutoka ndani ya shirika hilo zinasema kuwa shughuli za shirika hilo kubwa kuliko yote yanayojihusisha na hifadhi ya jamii nchini, haziendi kutokana na kutokuwapo na mtu aliyepewa jukumu la kukaimu nafasi hiyo.

Miongoni mwa mambo hayo ni ufunguzi wa Daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam ambalo lilitakiwa lianze rasmi kutumika Machi Mosi, ununuzi wa magari ya ofisi za mikoa, mkutano wa wanachama wa mwaka pamoja na wiki ya NSSF ambayo hujumuisha mambo mbalimbali, kama shughuli za kijamii, maonyesho ya huduma za NSSF na michezo.

Juhudi za kumpata Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama, anayehusika na mifuko ya hifadhi ya jamii hazikufanikiwa. Pia, Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue, ambaye amekuwa akitoa taarifa za uteuzi unaofanywa na Rais, hakupatikana jana.

Wiki iliyopita, Balozi Sefue alisema maswali kuhusu uteuzi wa kaimu yaelekezwe kwa Mhagama, ambaye alieleza wakati huo kuwa utaratibu wa kuimpata kaimu unaendelea.
 Kwa mujibu wa ripoti ya fedha ya mwaka 2011, shirika hilo lilikuwa na wanachama 501,218, kati yao wafanyakazi waliosajiliwa waliongezeka kutoka 17,666 hadi 18,779, sawa na ongezeko la asilimia 6, huku michango ikiongezeka kutoka Sh300.08 bilioni hadi Sh356.5 bilioni kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.8.

Kwa mujibu wa muundo wa uongozi wa NSSF, Mkurugenzi Mkuu ndiye kiongozi mkuu wa shirika akiwa na wakurugenzi wanane chini yake. 
Wakurugenzi hao wanahusika na uendeshaji (DO); utawala na rasilimali watu (DHRA); mipango, uwekezaji na miradi (DPIP); fedha (DF); teknohama (DIT); ukaguzi wa ndani (DIA); uthibiti na usalama wa mali (DARM) na huduma za kisheria (DLS).