YANGA SC imezidi kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya 2-2 na Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga SC kuendelea kuwa kileleni ikifikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 17, mbele ya Azam FC na Simba SC wenye pointi 39 kila mmoja.
Azam FC wao wana viporo viwili, huku Simba SC wakicheza mechi 17 kama Yanga.
Watoto wa Jangwani ndio walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake , Amissi Tambwe aliyefunga goli kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.iliwachukua dakika chache Prisons wakasawazisha bao hilo kupitia kwa Jeremiah Juma Mgunda aliyefunga kwa kichwa dakika ya 40 akimalizia krosi ya Mohammed Mkopi.
Mkopi akaifungia Prisons bao la pili dakika ya 62 kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo wa zamani wa Yanga SC, Juma Seif Kijiko.
Simon Msuva alitokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Deus Kaseke aliisawazishia Yanga kwa mkwaju wa penati dakika ya 84 baada ya Meshak Suleiman kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.hadi mwamuzi anamaliza dakika 90 ya mchezo yanga 2 prisons 2.