Jumanne, 9 Februari 2016

Adhabu Ya Kifungo Cha Nje Kwa Mujibu Wa Sheria Ya Huduma Kwa Jamii

Kwa mujibu wa kifungu na 3(2) (a) cha Sheria ya Huduma kwa Jamii ya mwaka 2002 kifungo cha nje ni utaratibu ambao unampa fursa mfungwa kutumikia kifungo chake nje ya gereza kwa kufanya shughuli/kazi zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii.
 
Utaratibu huu hutolewa kwa wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miaka mitatu bila kujali wana faini au hawana. Wapo wahalifu wanaohukumiwa moja kwa moja mahakamani kwenda kutumikia kifungo cha nje na wengine huingia gerezani kwanza na baadaye utaratibu wa maombi maalum hufanyika ili mfungwa husika kwenda kutumikia kifungo kwa utaratibu huo.
 
Sheria ya Magereza Sura ya 58 kifungu Na. 52 (1) (2) inatoa utaratibu wa kumuondoa mfungwa aliyepo gerezani huku akiwa ana sifa ya kutumikia kifungo chake kwa utaratibu wa huduma kwa jamii.
 
Kifungu hicho cha Sheria kinaeleza kuwa pale ambapo Mkuu wa gereza atajiridhisha kuwa kuna mfungwa ambaye ana sifa ya kutumikia kifungo chake chini ya utaratibu wa huduma kwa jamii, atamshauri mfungwa huyo juu ya utaratibu huo kwa kuzingatia sifa alizonazo na ikiwa mfungwa huyo ataridhia kuachiliwa kwake katika utaratibu wa huduma kwa jamii, Mkuu wa Gereza atawasilisha maombi maalum katika Mahakama iliyomfunga kwa ajili ya maandalizi ya kuachiliwa kwa mfungwa huyo katika utaratibu wa huduma kwa jamii.
 
Mahakama baada ya kupokea maombi hayo, itafanya uchunguzi kulingana na kifungu Namba 3 cha Sheria ya Huduma kwa jamii na ikijiridhisha kuwa mfungwa husika ana sifa za kutumikia katika utaratibu wa Huduma kwa jamii, Mahakama husika itatoa amri ya kuachiliwa kwa mfungwa huyo chini ya utaratibu huo.
 
Aidha, Usimamizi na Utekelezaji wa adhabu hii husimamiwa na Idara inayojitegemea ya Huduma kwa Jamii iliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
 
Mfungwa anayetumikia kifungo cha nje ni lazima aishi kwa kufuata Sheria na masharti aliyopangiwa. Masharti hayo ni kuwa chini ya uangalizi maalum, kutoondoka nje ya Mkoa bila kibali na kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka muda wake wa kifungo chake utakapokamilika.
Imetolewa na;
Lucas Mboje, Mrakibu Msaidizi wa Magereza,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
DAR ES SALAAM
09 Februari, 2016