Jumatatu, 13 Julai 2015

Hatimaye dr magufuli atangazwa kupeperusha bendera ccm katika kuwania urais


Dk John Magufuli ameteuliwa kupeperusha bendera ya chama cha mapinduzi kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu huku akimteua Mh Samia Hasan Suluhu kuwa mgombea mwenza.

Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi huo spika wa bunge Mh Anne Makinda amesema Dk Magufuli amewabwaga wagombea wengine wawili kwa kupata 2104 sawa na asilimia 87.1 ya kura zote zilizopigwa zilikuwa 2422 ambazo kati hizo kura sita zimeharibika.
 
Mara baada ya Dk Magufuli kutangazwa wagombea wawili walioshindwa ambao ni Dk Asharoze Migiro na balozi Amina Salum Ally wamepata fursa ya kuhutubia mkutano mkuu wa chama hicho ambapo mbali na kuwashukuru wajumbe wameahidi kumuunga mkono mgombea urais aliyeteuliwa na chama chao huku wakielezea mchakato ulivyokuwa mgumu.
 
Kwa upande wake Dk Magufuli amewahidi watanzania kuwa hatawaangusha na ameupokea uteuzi huo kwa mikono miwili na kuwaomba viongozi na wana CCM kumuunga mkono kwa kumpa ushirikiano ili aweze kulivusha taifa dhidi ya umaskini na hapohapo akamtaja Mh Samia kuwa mgombea mwenza wake.
 
Rais wa Zanzibar Dk Ally Mohamed Shein ambaye ameteuliwa kwa mara ya pili kupeperusha bendera ya chama hicho kwa upande wa visiwani humo ameelezea mafanikio yaliyopatikana wakati wa awamu ya kwanza ya uongozi wake.
 
Mwenyekiti wa chama hicho rais Jakaya Kikwete mbali na kumuelezea magufuli kuwa ni mtendaji hodari amewasihi wanaccm kutenda haki katika kura za maoni ndani ya chama wakati wa kuchagua wagombea ubunge na udiwani ili aweze kupata watu wataomsaidia kwenye utendaji wake  na kuwataka waliopata majeraha ya kutokuteuliwa kutokukata tamaa.