Jumanne, 28 Aprili 2015

AFC Bournemouth Waungana Na Watford Kucheza EPL


Usiku wa kuamkia hii leo AFC Bournemouth iliungana na klabu ya Watford katika safari ya kucheza ligi kuu ya soka nchini England, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Bolton Wanderers.
Ushindi huo umeiwezesha AFC Bournemouth kufikisha point 84 pamoja na tofauti ya mabao 50 kufunga na kufungwa huku mchezo mmoja ukisalia katika ligi daraja la kwanza nchini England.
Hata hivyo ukiangalia msimamo wa ligi hiyo utajiaminisha kwamba klabu ya Middlesbrough ina uwezo wa kufikisha point 84 endapo watashinda mchezo wao wa mwishoni Brighton & Hove Albion, kwa kuiombea AFC Bournemouth kupoteza mchezo wao dhidi ya Charlton Athletic.
Lakini ukiangalia kwa umakini msimamo wa ligi daraja la kwanza nchini England utabaini kwamba AFC Bournemouth wamepanda daraja kwa faida ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na kama itakua tofauti na hapo, basi Middlesbrough wanaoshika nafasi ya tatu kwa sasa, itawalazimu kusaka ushindi wa mabao 21 katika mchezo wao wa mwisho.
Watford walitangulia katika safari ya kucheza ligi kuu ya soka nchini England baada ya kufikisha point 88 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi daraja la kwanza.
Hata hivyo bado nafasi moja ya kucheza ligi kuu msimu ujao imesalia, na itazihusu klabu za Middlesbrough, Norwich City, Ipswich Town, Derby County ambazo zitacheza michezo ya mtoano na kuwapata wababe wawili watakaocheza mchezo wa fainali na kumpata shababi mmoja atakaejiunga na AFC Bournemouth na Watford.
Kanuni za ligi kuu ya soka nchini England, huzishusha timu tatu za mwisho na kutoa nafasi kwa timu tatu kutoka ligi daraja la kwanza kucheza ligi hiyo msimu unaofuata.