Jumatatu, 4 Mei 2015
WAZIRI MKUU AUNDA KAMATI YA KUDUMU KUSIMAMIA USAFIRI WA BARABARANI NCHINI
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Peter Mizengo Pinda, ameunda Kamati ya Kudumu ya kusimamia usafiri wa barabarani nchini.
Akizungumza na Wandishi wa habari jijini Dar es salaam leo,Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Samweli Sitta amesema lengo kuu la kuundwa kwa Kamati hiyo ni kutokana na kuwepo kwa mvutano baina ya wadau wanaohusika na usafiri wa Barabarani, madereva na waajiri wao hali inayosababisha kutokea kwa migomo ya mara kwa mara.
Mgomo wa madereva uliibuka tena leo baada ya mabasi na magari ya mizigo kugoma tena kwa mara ya pili kwa lengo la kushinikiza kutatuliwa madai yao ambayo awali baadhi ya viongozi wakuu wa Serikali walijaribu kutatua mgogoro wao ambapo hata hivyo hawakufikia suluhu.