Alhamisi, 7 Mei 2015

Uchawi Bagamoyo: Jini lawahamisha Wananchi kijijini


Mji wa kihistoria Bagamoyo ambao umekuwa ukitembelewa na watu mbalimbali wakiwemo watu kutoka nje ya Tanzania wamekuwa wakifika na kuona mambo ya kale, umeendelea kuzalisha habari na matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwaacha watu na alama za mshangao!
Mara kadhaa kumeripotiwa matukio mengi ambayo pengine hayajawahi kuripotiwa sehemu nyingine yoyote ndani na hata nje ya mipaka ya Tanzania.
Mwaka jana kuliripotiwa tukio la mwanamke mmoja kujifungua hirizi baada ya kubeba mimba kwa miezi tisa wakati juzi kumeripotiwa tukio la binti swa miaka 20 kudaiwa kujifungua Nazi pia baada ya ujauzito wa miezi tisa!
Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Pande huko huko Wilayani Bagamoyo ndani ya Mkoa wa Pwani, wamelazimika kuhama nyumba zao baada ya kudaiwa uwepo wa mtu asiyeonekana ambaye amekuwa akiwatokea nyakati za usiku na kuwakaba huku wengine wakishambuliwa kwa kupigwa makofi!
Taarifa zilidai kwamba, mtu huyo ambaye kwa sasa amekuwa kero kubwa kwa wananchi hao, amekuwa akijitokeza nyakati za usiku pekee na kuwakaba baadhi ya wananchi pamoja na kuwajeruhi.
Opya Buguza, mkazi wa kijiji hicho cha Pande, alisema kuwa, mtu huyo ambaye anamfano wa kitu kama ‘Jini’ amekuwa akitokea kijijini hapo mara kwa mara na ingawa waganga wamekuwa wakifika na kumwondoa lakini amekuwa akirudi kila mwaka.
“Mimi nahisi kuna mtu hapa kijiji atakuwa amemtengeneza kwa ajili ya manufaa yake lakini sasa amemshinda na amekuwa kero hapa kijijini! Watu hatuna raha hasa nykati za usiku na imefikia mahala watu wanashinda hapa kijijini mchana ukifika usiku wanahama na kwenda kulala kijiji cha jirani cha Mbegani na kurejea siku inayofuata,” anasema Buguza.
Anasema mtu huyo wa ajabu hivi karibuni alimjeruhi mtoto mdogo aliyekuwa amelala na kusababisha majeraha ambapo wazazi wake walimchukuwa na kumkimbiza kwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Juzi pia alimtokea bibi yangu na kumkaba, bibi akapiga kelele lakini tulivyokwenda akakimbia na kumkuta bibi akiweweseka! Baada ya hapo tukamchukuwa bibi na kwenda kulala nae chumbani kwangu,” anasema.
Aidha, mzee Mohammed Mnandari (65) maarufu kama Abobo anasema hivi karibuni alimtokea usiku na kumkalia begani ambapo mbali na kumjeruhi alimwacha na majeraha kadhaa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Akithibitisha kutokea na tukio hilo, Mwenyekiti serikali za mitaa Bw. Salum Mlalikwa alisema ni kweli tukio hilo lipo kijijini hapo na linafanywa na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho ambao hawapendi maendeleo yanayoletwa na serikali.
Alisema wapo wananchi waliotamka wazi kwamba hakuna maendeleo yatakayopatikana kijijini hapo na katika kuhakikisha hilo linafanikiwa wameapa kuwa Bandari ambayo kwa sasa serikali inapambana kuhakikisha inajengwa kijijini hapo, haijengwi!
“Ni wananchi wachache tu wasiopenda maendeleo ndio wanafanya haya ili kuzikatisha jitihada za serikali katika kutuletea maeneleo. Na watu hao wameapa kutojengwa bandari hapa…lakini mimi kama mwenyekiti nitapambana kuhakikisha bandari inajengwa kijijini hapa hata kama wametengeneza majini kuitisha serikali,” alisema Bw. Mlalikwa.
Tayari baadhi ya wananchi wakishirikiana na baadhi ya wazee kijijini hapo wameita mganga wa kienyeji kwa ajili ya kuondoa kadhia hiyo.