Ijumaa, 8 Mei 2015
JUMA NYOSO OUT MCHEZO WA KESHO NA POLISI
Mlinzi wa kutumainiwa wa Mbeya City Fc, Juma Nyosso ataukosa mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara dhidi ya Polisi Morogoro unaotarajiwa kuchezwa kesho jumamosi kwenye uwanja wa Sokoine kufuatia kadi tatu za njano alizoonyeshwa kwenye michezo iliyopita.
Akizungumza kocha mkuu wa mbeya city Juma Mwambusi amesema kuwa Nyosso alipata kadi za njano tatu mfululizo kwenye michezo iliyopita hivyo ni wazi hatakuwa sehemu ya kikosi jumamosi hii.
“Nahodha wetu (Nyosso) ataukosa mchezo wa jumamosi hii ni kutokana na kadi tatu za njano, alipita mfululizo kwenye michezo iliyopita, ni pigo kumkosa kwenye mchezo muhimu kama huu lakini hatuna wasiwasi kwa sababu tayari tushaandaa vijana wengine kuziba pengo lake na imani yangu kubwa watafanya kazi nzuri” alisema.
Kuhusu mchezo wa jumamosi kocha Mwambusi amesema kuwa maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika kinachosubiriwa ni siku ya mchezo tu City iingie uwanjani kutafuta matokeo.
“Kwetu sisi kila kitu kimekamilika, tunasubiri siku ya mchezo tu, hizi zitakuwa dakika 90 zingine muhimu kwetu kwa sababu tunahitaji matokeo ili kusalia kwenye nafasi ya nne, hili linawezekana, tulianza ligi vibaya lakini tukaweka malengo ya kumaliza kwenye nafasi tano za juu na hili litatimia” alimaliza.