Ijumaa, 1 Mei 2015

Mugabe: Wazuieni watu wenu kwenda Afrika Kusini

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anayataka ya Afrika kuwazuia raia wake kuhamia Afrika Kusini kwa shabaha kukimbilia ajira ili kudhibiti vitendo vya vurugu dhidi ya wahamiaji nchini humo. 

Wimbi la vurugu za wanaopinga wageni nchini Afrika Kusini limegharimu maisha ya watu saba katika mji ya Durban na Johannesburg katika kipindi cha wiki nne zilizopita. Hata hivyo serikali ya taifa hilo imepeleka vikosi vya jeshi katika mitaa hiyo kudhibiti wimbi hilo.
Baada ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa yaliyo kusini mwa Afrika (SADC) kufanya majadiliano kuhusu maendeleo ya kiviwanda katika eneo la kusini mwa Afrika, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aliwaambia waandishi wa habari kwamba rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma aliwapa taarifa fupi viongozi wa kanda hiyo kuhusu vurugu zilizotokea.
Zuma aliuambia mkutano huo kwamba serikali yake itatoa elimu kwa umma kuwa wastahimilivu kwa wageni na ataviweka vyombo vya usalama vya taifa hilo katika hali ya tahadhari kwa wakati wote kwa lengo la kudhibiti mashambulizi ambayo yanaweza kujitokeza.
Nikimunukuu hapa rais Mugabe ambae ndiye mwenyekiti wa sasa wa SADC alisema " Napendekeza kwamba sisi, majirani, lazima tufanye kila liwekezekanalo kudhibiti watu zaidi kwenda Afrika Kusini. Kama tutaweza kufanikisha hilo, tunaweza pia kuwaresheja wale walioko katika taifa hilo nyumbani".
Mwenyekiti huyo wa sasa wa SADC, aliendelea kusema jukumu kufanikisha watu waliopo katika taifa hilo kurejea nyumbani si la Afrika Kusini pekee bali kwa mataifa yote jirani. Na kuongeza kuwa watu katika kanda hiyo wasiwe na shauku ya kukimbilia Afrika Kusini.
 
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na mwenzake wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, mjini Harare.
Inakadiriwa raia milioni moja wa Zimbabwe wanaishi Afrika Kusini, baada ya kuikimbia hali ya kuzorota kwa uchumi na vurugu za kisiasa miaka kumi na tano iliyopita. Hata hivyo tayari Zimbabwe imefanikisha kurejeshwa raia wake wapatao 800 kutoka Durban, lakini idadi kubwa ya hao wameonesha ishara ya kutaka kurejea Afrika Kusini, taifa ambalo lina ushirikiano mkubwa wa kibashara na Zimbabwe.
Mugabe ambae ameitawala Zimbabwe tangu kupata uhuru wake kutoka kwa mamlaka ya zamani ya koloni la Uingereza 1980 amesema watu wanaoelezewa kama wimbi la uhamiaji nchini Afrika Kusini hawaendi huko kwa shinikizo la serikali zao. Amesema ni watu wanaokwenda kwa ridhaa yao kwa kufikiria Afrika Kusini ni pepo ya eneo la kusini mwa Afrika.
Wapinga wahamiaji nchini Afrika Kusini wamekuwa wakilalamikia tatizo la ajira. Taarifa rasmi ya serikali kuhusu tatizo hilo inaonesha kwamba lipo katika asilimia 25, ingawa wachumi wanasema kwa sasa ni kubwa zaidi ya takwimu hizo.
Rais Mugabe ameonesha kukubalina na hayo kwa kusema viwango vya maisha kwa Waafrika Kusini weusi na wageni wanaodhani kuna pepo katika taifa hilo ni duni sana na kuingia kwao huko kunafanya maisha kuwa mabaya zaidi.