Ijumaa, 1 Mei 2015

Mei Mosi – Je, wafanyakazi wana sababu ya kusherehekea?



KILA mwaka Mei Mosi huadhimishwa kama Siku ya Wafanyakazi duniani. Ni sikukuu ya kimatifa inayoadhimishwa na waajiriwa wanaovuja jasho na kuzalisha mali na huduma kwa ajili ya waajiri au matajiri wao.
Tanzania ni kati ya nchi zinazosheherekea Siku hii kwa maandamano na mikutano inayohutubiwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wakuu wa serikali kama mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya au hata na mkuu wa nchi.
Nikiangalia jinsi siku hii ya Mei Mosi (wengine wanaita Mei Dei) ilivyo na shamra shamra na tafrija, ninakuwa na hisia kuwa imetekwa nyara na waajiri.
Tuna Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) lakini sioni ishara kuwa limeotesha mizizi yake miongoni mwa wafanyakazi. Ndiyo maana unakuta katika nchi hii yenye watu milioni 45 tunaambiwa TUCTA lina wanachama 350,000 tu na kule Zanzibar ZATUC lina wanachama 15,000 tu!
Ndiyo maana inapofika siku hii utakuta maandalizi rasmi yakifanywa na TUCTA  na vyama vya wafanyakazi. Lakini si maandalizi ya kuwashawishi na kuwahamasisha wafanyakazi wajitokeze na kujiunga, bali mawasiliano hufanywa na wakuu wa mashirika na makampuni “wawawezeshe” waajiri wao ili wahudhurie.
Ndivyo nilivyoona pale Chuo cha Usimamizi wa Fedha miaka ile ya 1970, 1980, na 1990 wakati wa Juwata na OTTU (wakati ule) zilivyokuwa zikifanya kazi kwa kuwezeshwa na menejimenti.
Sikumbuki kama tulitembelewa na wakuu kutoka makao makuu waliotaka kujua shida zetu, bali wakuu wa tawi letu walituita mara kwa mara na “kutuelimisha” kuhusu nidhamu ya kazi. Mishahara yetu ikikatwa bila ya ridhaa yetu ili kutunisha mfuko wa chama. Nasikia mtindo huu unaendelea hadi leo.
Na ndivyo siku hii ya Mei Mosi inavyoadhimishwa kwa bendera, mashati, kofia, miavuli, miziki na tafrija iliyolipiwa na waajiri. Kwa vile TUCTA haitangazi bajeti yake tunapaswa tujiulize ni fedha kiasi gani zinatumika. Kiasi gani zinatokana na TUCTA, serikali, makampuni, waajiri na wachangiaji binafsi.
Tunapozungumzia siku hii ya Mei Mosi ni vizuri kusisitiza kuwa hii ni siku ya kimataifa. Ni vizuri kuangalia chimbuko lake na jinsi ilivyoanza mpaka kufikia ilivyo hii leo.
Kwani si wengi wanaoelewa ya kuwa sikukuu hii ilizaliwa karne ya 19 huko Marekani, nchi ambayo leo ni kitovu cha ubepari (au ubeberu) ulimwenguni. Kutoka huko wazo hilo lilienea Ulaya na kisha ulimwenguni kote.
Wakati huo dai kubwa la wafanyakazi lilikuwa ni kupinga muda mrefu wa kazi na haki ya kujumuika. Wakati huo ilikuwa kawaida kwa wafanyakazi kufanyishwa kazi kuanzia alfajiri hadi usiku, yaani saa 14 au hata 18 kwa siku. Wengine walifanya kazi hata saa 20 kwa siku. Hali ya kazi ilikuwa hatarishi mno kiasi kwamba matajiri hawakujali wafanyakazi wanapojeruhiwa au kufa wakiwa kazini. Ilikuwa kawaida kwa wafanyakazi kufa wakiwa na umri mdogo kutokana na magonjwa yaliyosababishwa na mazingira duni kazini.
Mnamo 1827 mjini Philadelphia wafanyakazi waliunda chama chao cha kwanza. Lengolao lilikuwa kudai saa za kazi zisizidi 10 kwa siku. Mwaka 1834 wakaitisha mgomo wao wa kwanza. Tayari wafanyakazi wa Uingereza na Australia walikuwa wanadai saa nane kwa siku.
Dai hili likawa ni la kimataifa na ndilo likaibua wazo la Mei Mosi kuwa siku ya wafanyakazi wote duniani. Tarehe 20 Agosti 1866 mjini Baltimore (Marekani) walikusanyika wajumbe kutoka vyama 30 vya wafanyakazi nao wakaamua kuunda shirikisho lao (National Labor Union).
Mwamko na mshikamano huu wa wafanyakazi ulienea katika nchi nyingi hadi mwaka 1869 ukaitishwa mkutano mkuu wa kimataifa nchini Uswisi. Huo ndio mwanzo wa shirikisho la kimataifa. Mwaka 1876 mkutano mwingine wa kimataifa ulifanyika mjini Paris na uamuzi ukafikiwa wa kuteua Mei Mosi kama Siku ya Wafanyakazi duniani.
Mwaka 1884 shirikisho la vyama vya wafanyakazi wa Marekani (American Federation of Labour) liliitisha mkutano mkuu. Azimio likapitishwa kuwa kufikia Mei Mosi 1886 kikomo cha saa nane kwa siku kingetungiwa sheria la sivyo migomo ingeitishwa nchini kote.
Baadhi ya wanaharakati waliona madai haya ya saa nane hayatasaidia sana, kwani bado unyonyaji, udhalilishwaji na maisha duni yangeendelea hata baada ya sheria hiyo kupitishwa. Walisema“Mfanyakakzi ataendelea kuwa mtumwa hata kama anafanya kazi saa nane kwa siku”. Wao walitaka mabadiliko ya kimfumo ili wafanyakazi wadhibiti njia kuu za uzalishaji ili kuondoa unyonyaji wa kibepari.
Wengine waliona ni vizuri madai yao yaendelee kwa hatua. Ndiyo maana ilipofika Mei Mosi 1886 zaidi ya wafanyakazi 300,000 kote Marekani waligoma kufanya kazi na wakajiunga na maandamano ya kitaifa. Haya ni maandamano ya kwanza ya aina yake kufanyika siku ya Mei Mosi.
Polisi walitumia nguvu za dola kuzuia maandamano ambayo yaliendelea hadi siku ya Mei tatu, hasa katika mji wa Chicago. Polisi wakatumia risasi za moto na marungu kuwashambulia waandamanaji. Wafanyakazi saba wakauawa na wengi zaidi ya 40 wakajeruhiwa. Watu wenye hasira wakawashambulia polisi ambao pia waliuawa katika uwanja wa Haymarket. Watu saba wakafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa.
Wakati wa kuonyongwa mmoja alijiua kwa kujilipua. Ulimwengu ulijawa na hasira kwa hukumu hii iliyopitishwa fasta fasta.
Na nchini Canada nako harakati za kifanyakazi zilipamba moto mnamo Aprili 1872 wakati wafanyakazi wa Toronto walipofanya maandamano makubwa ili kudai kufunguliwa kwa viongozi wao 24 waliofungwa kwa kuhimiza mgomo wa kudai saa nane za kazi kwa siku. Wakati huo vyama vya wafanyakazi na migomo ilikuwa ni marufuku.
Hata hivyo, maandamano ya halaiki yaliendelea na serikali ikalazimika kurudi nyuma. Waziri mkuu wa Canada akalazimika kufuta sharia iliyokataza vyama vya wafanyakazi.
Ilipoingia karne ya 20 serikali ya Marekani ilifanya kila jitihada kuzuia maandamano ya Mei Mosi. Mbinu moja ilikuwa ni kutangaza siku hiyo kama siku ya “sheria na utulivu” lakini wafanyakazi waliendelea kuiita Mei Mosi au siku ya mfanyakazi.
Mbinu nyingine waliyofanya ni kubadilisha tarehe. Badala ya Mei Mosi ikawa ni siku ya Jumatatu ya kwanza ya Septemba. Hii ndiyo Mei Mosi mbadala Marekani na Canada ambako tarehe imebadilishwa ili kuepukana na mshikamanao wa kimataifa.
Na Tanzania nako wafanyakazi na vyama vyao wana historia ndefu na adhimu ya kupigania haki zao tangu wakati wa ukoloni. Chini ya utawala wa kikoloni tulikuwa na shirikisho la TFL Tanganyika huku Visiwani kukiwa na FPTU na ZPFL. Vyama hivi vya wafanyakazi vilikuwa ni vya kimaendeleo na msitari wa mbele kupigania uhuru na mapinduzi nchini. Je, historia hii inaendelea?
Leo kuna TUCTA na ZATUC. Mei Mosi inaadhimishwa kila mwaka na mwaka huu hali kadhalika kutakuwa na shamra shamra. TUCTA itatoa madai kama kawaida ya mshahara kima cha chini shilingi 750,000, msamaha wa kodi pamoja na serikali kuwalipa walimu Sh. 49 bilioni wanazodai zikiwamo Sh.30 bilioni walizopunjwa katika mishahara yao. Na wakuu wa serikali nao (pamoja na Rais) wataahidi kuboresha maisha ya wafanyakazi.
Nimesema TUCTA haielekei kuwa na mizizi miongoni mwa wafanyakazi, haina uhusiano wa karibu na mfanyakazi aliye mahali pa kazi. Chama kipo kisheria. Nguvu zake zinatokana na sheria. Ndiyo uhalali wake. Ndiyo maana mara nyingi wafanyakazi wanatoa madai yao nje ya TUCTA ambayo inashitukizwa na kuachwa kwenye mataa. Si ajabu utasikia wafanyakazi wa benki au waalimu wanatangaza kuunda vyama vyao nje ya TUCTA. Hii imeonekana katika Mei Mosi zilizopita wakati kunakuwa na makundi mawili ya maandamano.
Karibuni Rais Jakaya Kikwete alikutana na wakuu wa TUCTA, Ikulu. Akaagiza uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi katika utumishi wa umma. Najiuliza kwa nini hatuna mabaraza hayo katika kampuni binafsi. Sina hakika TUCTA ina matawi mangapi katika makampuni.
Mkutano wa Ikulu ulidumu kwa muda wa saa 10 na ulihudhuriwa na vyama shirikishi vya TUCTA pamoja na vigogo wa serikali. Tunaambiwa walijadili “jinsi ya kutafuta njia za kuboresha maslahi na ustawi wa wafanyakazi nchini”.
Tunaambiwa walijadili hali ya afya ya wafanyakazi katika migodi mbalimbali nchini. Sina hakika kama walijadili pia ripoti iliyotolewa na shirika la kimataifa (HRW) kuhusu watoto wanaoajiriwa katika machimbo ya dhahabu nchini.
Katika utafiti wao HRW waliwahoji wafanyakazi zaidi ya 200, wakiwamo watoto 61, katika migodi midogo 11 iliyopo katika Mikoa ya Geita, Shinyanga na Mbeya.
Ripoti hii ya kurasa 96 inafanana na hali iliyokuwa miaka zaidi ya 100 iliyopita huko Marekani na Ulaya. Leo hapa Tanzania tunazungumza  jinsi maelfu ya watoto kuanzia umri wa miaka minane wanavyofanyishwa kazi kwa muda wa saa 24 katika migodi, wanapumua vumbi lenye sumu na wanatumia zebaki ambayo inafupisha maisha yao. Mgodi ukiporomoka basi maisha yamepotea.
Watafiti wa HRW wanaitaka serikali yetu itekeleze sheria ya kitaifa na ya kimataifa inayokataza ajira ya watoto migodini. Pia inawaomba wafadhili waihimize serikali. Ripoti kama hii pia imeandikwa na mtafiti kutoka Uingereza.
Yeye anasema leseni ya uchimbaji hutolewa kwa mwekezaji wa ndani na nje ambaye anaahidi mshahara. Mwisho wa mwezi mtoto anaambulia patupu au anapewa pesa kiduchu. Akilalamika anaambiwa kazi hakuna. Wengi wanasema mfumo mzima unawafanya wawekezaji wawe na uwezo kamili wa kuamua bila ya kuingiliwa na serikali. Ni matajiri wa kupindukia na wana uwezo wa kuwahonga maofisa. Wafanyakazi nao wanazibwa midomo kutokana na uoga.
Je, TUCTA wanaelewa hayo au wanasubiri tu waalikwe Ikulu? Je, katika risala zao wanagusia hali ya watoto wetu wanaoteseka katika migodi ya dhahabu?
Tusiwe tunafurahia tu utajiri wa nchi yetu na kudai Tanzania ni nchi ya nne katika uzalishaji wa dhahabu barani Afrika, ilhali wazalishaji wetu wanatendewa unyama. Ni dhuluma ya aina hii ndiyo iliyowafanya wafanyakazi wafungwe na wauawe miaka zaidi ya mia iliyopita huko Marekani.
Ni dhuluma hii ndiYo iliyowafanya wafanyakazi hao watangaze siku ya Mei Mosi kuwa siku ya mshikamano, siku ya kudai haki zao.