Ijumaa, 1 Mei 2015

DABI MBEYA NI PATASHIKA NGUO KUCHANIKA JUMAMOSI HII TZ PRISONS NA MBEYA CITY



Jumamosi hii kwenye uwanja wa Sokoine jijini  Mbeya ‘utapigwa’ mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara ambao utazikutanisha timu mbili kutoka jiji hili kubwa katika eneo  la  nyanda za juu kusini yaani Mbeya City Fc  na Tanzania Prison.
Huu ni mchezo  wa nne  kwa timu hizi kukutana uwanjani  awali mara mbili kwenye msimu uiopita na mara moja mzunguko wa kwanza  na  jumamosi  hii itakuwa mara pili katika msimu huu hivyo kukamilisha  michezo minne.
Msimu uliopita City ilifanikiwa kushinda michezo yote miwili ikiwa ni  ushindi wa bao 2-0, yaliyofungwa na Peter Mapunda dakika ya 67 na Deogratius Julius dakika ya 79, katika mchezo wa kwanza na 1-0  mzunguko wa pili bao lililofungwa na Paul Nonga
Kwa maana hiyo Mbeya City itaingia kucheza mchezo wa jumamosi ikiwa  mbele kwa kushinda mara mbili katika michezo mitatu  huku Prison wakiingia uwanjani wakijivunia sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo wa kwanza msimu huu  kwa mabao yaliyowekwa kimiani na Paul Nonga na Temi Felix kwa upande wa City  huku Boniface Hau na  Nurdin Chona wakifunga upande wa Prison mchezo uliochezeshwa na mwamuzi  Simon Mbelwa wa Pwani.
Ukitizama kwa makini unaweza kugundua kuwa mchezo huu ni tofauti kabisa na iliyotangulia hapo awali kwa sababu umekuja kwenye wakati ambao kila timu inahitaji matokeo ili kusogea sehemu nyingine kwenye msimamo wa ligi, kwa vyovyote vile utakuwa mchezo mgumu na wenye kila aina ya ushindani.
City inahitaji matokeo ili kuendelea kujikita kwenye nafasi ya nne  iliyopo sasa kwenye msimamo wa ligi,  huku Prison ikitafuta matokeo kujaribu kujipapatua mkiani kuepuka kushuka daraja huku ikichagizwa na ushindi iliyoupata juma lililopita kwa ‘kuidabisha’Mgambo Shooting ya Tanga  mabao 2-0.
Kuelekea Mchezo huo Kocha Juma Mwambusi amesema  huu ni mchezo muhimu pengine kuliko yote iliyopita  kwa sababu matokeo kwenye mchezo huo yataihakikishia City kuchukua nafasi ya nne ambayo pia wadhamini wa ligi hutoa zawadi kwa timu inayokuwa imefanikiwa kushika nafasi hiyo.
“Ni mchezo muhimu na mgumu kulingana na mazingira halisi kwa timu zote mbili, kwetu sisi ni muhimu zaidi kwa sababu tunahitaji nafasi ya nne ambayo  pia ina zawadi kutoka kwa mdhamini, tunafahamu ndugu zetu wako kwenye wakati mgumu zaidi na wanataka kuepuka kushuka daraja lakini bahati mbaya kwao nasi tunahitaji  hiyo nafasi kwa maana hiyo hizi zitakuwa ni dakika 90 ngumu kuliko zote  zilizowahi kutukutanisha” alisema.
Licha ya kujigamba kushinda Kocha wa Prison Mbwana Makata ana wasiwasi mkubwa  kuhusu uwezo wa kikosi cha Mbeya City Fc hasa ukizingatia  ushindi mzuri wa mabao 2-0 katika michezo iliyopita  lakini ameapa kupambana  kutafuta matokeo.
“Mbey City ilipata matokeo dhidi ya Simba na Kagera Sugar, hili jambo ambalo limetustua lakini tuko tayari kupambana muda wote wa mchezo hiyo jumamosi na tunataka kushinda ili tuwe kwenye nafasi nzuri” alisema Makata.