Jumapili, 5 Juni 2016

UMOJA WA MATAIFA WAPONGEZA UTENDAJI WA RAIS MAGUFULI


SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limeeleza kuridhishwa kwake na utendaji wa Rais John Magufuli katika mapambano ya rushwa, kuongeza uwajibikaji na ukusanyaji wa mapato.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Alvaro Rodriguez, alisema hayo jana katika semina ya wabunge kuhusu Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Dunia.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikipambana na rushwa na kusimamia kwa karibu ukusanyaji mapato, hali aliyosema itasaidia maendeleo kwa kuwa hakuna nchi iliyoendelea bila kuchapakazi.

Rodriguez alisema mbali na kuona maendeleo katika baadhi ya mikoa na mitaa, ameona jitihada hizo za Serikali na amefurahishwa na kuridhika nazo.

Mwakilishi huyo pia alisema Serikali ya Tanzania na Ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN), zimekuwa zikifanya kazi pamoja katika harakati za usambazaji wa malengo ya dunia kwa Watanzania.

Alisisitiza umuhimu wa malengo hayo kueleweka kwa wabunge, ili katika jukumu lao la kuisimamia Serikali, wawe mabalozi wa utekelezaji wa malengo hayo katika ufuatiliaji kwenye ngazi zote za utawala.

Awali akifungua semina hiyo, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliwataka wabunge kuoanisha malengo hayo na malengo ya Dira ya Taifa ya 2025 pamoja na malengo ya Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano wa 2016/2017 mpaka 2020/2021 ambao ulishafikishwa bungeni.

Dk Tulia aliwataka wabunge kila mmoja kuyaelewa vizuri malengo hayo ili kila mmoja ashikilie mahali atakapofuatilia Serikalini wakati wa utekelezaji wake.

Miongoni mwa malengo hayo ni pamoja na kutokomeza umasikini wa kila aina, kufuta njaa kwa kuhakikisha kuna kuwa na uhakika wa chakula bora kwakuboresha kilimo endelevu, kuhakikisha watu wote wanakuwa na afya bora nakupata huduma za afya na kupunguza utofauti wa kipato.

Akitoa mada katika semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Paul Kessy, alisema Tanzania imeshiriki kwa kiasi kikubwa katika maandalizi ya malengo hayo na hivyo mchango wake kuwa sehemu ya maudhui ya malengo hayo endelevu kwa maslahi mapana ya taifa na watu wake.

Kwa mujibu wa Kessy, sehemu ya mchango wa Tanzania katika kuunda malengo hayo, ilikuwa ni kutaka malengo hayo yahakikishe kuwa baadhi ya masuala ambayo hayakukamilika katika utekelezaji wa Malengo ya Milenia yanazingatiwa katika malengo endelevu.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kupunguza umasikini, upatikanaji wa ajira na kukuza uwezo wa nchi masikini hasa katika maendeleo ya teknolojia.