KIKOSI kamili cha Mbeya City Fc kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiweka sawa tayari kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu ya soka Tanzania bara unatarajia kuanza ‘kutimua vumbi’ desemba 12 huku City ikipangwa kuanza na Mtibwa Sugar kwenye uwanja w Sokoine jijini Mbeya.
Mapema leo kwenye kambi ya City iliyopo chuo cha ualimu Tukuyu jijini hapa kocha mkuu Meja mstaafu Abdul Mingange ameuambia mtandao huu kuwa hali ya mazoezi yaliyoanza jumapili iliyopita ni nzuri kwa sababu wachezaji mwitikio wa wachezaji kuwahi kambini kama iliyokuwa imepangwa umekuwa mzuri hivyo kurahisisha programu zake kwenda vizuri.
“Mwitikio wa wachezaji kuwahi kambini umekuwa mzuri, hii imerahisisha sana programu zangu kwenda sawa mpaka sasa ni wachezaji 20 wameshafika hapa hivyo hali ni nzuri, kikosini wanakosekana Juma Kaseja, Haruna Moshi na Haruna Shamte ambao walikuwa na ruhusa maalumu na ninawatarajia watakuwa hapa baada ya siku mbili” alisema.
Akiendelea zaidi Mingange aliweka wazi kuwa ameamua kuanza kambi mapema ili kuhakikisha kikosi chake kinakuwa kwenye hali nzuri kabla ya kuivaa Mtibwa Sugar desemba 12 kwenye uwanja wa Sokoine huku akiweka matumaini ya kupata matokeo mazuri kwenye michezo ya mzunguko ujao kufuatia anguko la awamu ya kwanza.