Jumapili, 15 Novemba 2015

BAADA YA MWAMBUSI KUONDOKA MBEYA CITY YANENA

juma-mwambusi1

  • Ni takribani mwezi mmoja sasa tangu aliyekuwa kocha mkuu wa Mbeya City Fc (timu ya kizazi kipya) Juma Mwambusi alipotangaza rasmi kuachana na timu hii ili kwenda kujiunga na Young African ya Dar es Salaam ambayo pia inashiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara kama ilivyo City.
  • Kujiunga na Yanga, safari ya Mwambusi aliyedumu ‘kikosini’ takribani miaka mitano na kupatia mafanikio makubwa, ni wazi imekuwa na baraka tele kutoka kwa uongozi, wadau na mashabiki wa hasa kwa yote aliyoyafanya ndani ya timu hii, ndiyo maana mpaka leo hajawahi kukutana na kadhia yoyote kuhusu kuondoka kwake kikosini.
  • Kwa wadau wa soka, kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine kunakowakuwata wachezaji, makocha na kwa uchache viongozi ni jambo la kawaida ambalo linafanyika kwa lengo moja tu kuongeza mafanikio kwa pande zote zinazohusika, huku maslahi yakiwa ‘chagizo kuu’ kwa upande mwingine.
  • Safari ya kocha Mwambusi kutoka kwenye timu aliyoshiriki kuianzisha na kudumu nayo kwa miaka mitano kwenda timu nyingine hakika ni tiketi ya mwalimu mpya kuja kuliongoza bechi la ufundi la City kwa lengo la kusukuma mbele yote yaliyokwisha fanywa hapo kabla.
  • Kwenye hili ni bora ifahamike kuwa yapo maombi mengi ‘kupitiliza’ kutoka ndani na nje ya Tanzania yanayohitaji tiketi (nafasi) ya kuongoza benchi la ufundi la timu ya kizazi kipya huku Kinnah Phiri likiwa ndiyo jina linalotajwa sana na mashabiki wa timu hii kuwa ndiye mtu sahihi wa kuvaa viatu vya Mwambusi.
  • Kwa nini Kinnah Phiri..! huenda mashabiki hao wanaguswa na historia nzuri ya kocha huyu wa zamani wa Free State ya Afrika Kusini na raia wa Malawi aliyeanza kupata mafanikio ya soka akiwa mshambuliaji kwenye timu za Big Bullets ya nchini kwao pia Manzini Wanderers ya Swaziland ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kucheza michezo 30 na kufunga mabao 36 akiwa na jezi ya The Flames (timu ya taifa ya Malawi) 1974-1981.
  • Kutajwa sana kwa jina hili na mashabiki wa City ndiyo sababu ‘iliyomuinua kitini’ Katibu Mkuu wa City, Emmanuel Kimbe, kutoka mbele ya vyombo vya habari na kuzungumza juu ya hili akisema kuwa kwenye soka kuna mambo mengi wakati mwingine linalotarajiwa hukosekana na lisilotarajiwa hutokea.
  • “Baada ya kuondoka Mwambusi ni wazi nafasi ikabaki wazi, binafsi nimesikia juu ya kocha Phiri kwa muda mrefu ila naomba niseme mbele yenu kuwa kwenye soka kuna mengi, huyu ni kocha mzuri mwenye sifa zote yawezekana akawa au asiwe kikubwa ni uhitaji na aina ya uhitaji wenyewe” alisema.
  • Tuanzie hapo,’huyu ni kocha mzuri mwenye sifa zote’ sawa kwenye mlengo upi? Hilo ni swali lingine, imani iliyopo ni kuwa anatajwa sana kwa sababu ni mmoja wa makocha wenye uwezo wa kujenga kikosi cha nguvu na ushindani kinachoweza kupambana dakika zote 90 popote kwa lengo la kutafuta matokeo.
  • Novemba 25,2008 jarida moja la michezo huko Afrika Kusini lilindika habari iliyobebwa na maneno ‘Malawi yarejea kwenye ramani ya soka’ hii ni kufuatia mwanzo mzuri kwenye michezo ya awali kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika ambazo zilipangwa kuchezwa baadae huko Angola.
  • Akiwa kiongozi wa benchi la ufundi kwenye kikosi cha Free State ya Afrika Kusini kwa misimu minne tofauti alikuwa na matokeo ya kubadili nafasi kwenye msimamo PSL,kitu muhimu ni kuwa alifanikiwa kuijenga timu hiyo kutoka timu ya kawaida kuwa ya ushindani, huyo ndiyo Kinnah Phiri mwenye kivuli cha Mwambusi kutoka vinywa vya mashabiki wa City.
  • Tukimpisha kocha huyo na sifa zake,kwenye sentesi nyingine Katibu Mkuu wa City Emmanuel Kimbe alisema ni kweli bechi la ufundi limeondokewa na mtu muhimu lakini suala la kutafuta mbadala linahitaji utulivu mkubwa ili kumpata mtu sahihi atakae kwenda sawa na utamaduni wa timu.
  • “Nakiri wazi kuwa aliyeondoka alikuwa mtu muhimu hasa ukizingatia alishiriki katika kuianzisha timu lakini kwenye soka ndivyo ilivyo, kitu muhimu kwetu kwa sasa ni utulivu huku tukisaka mtu sahihi atakayeweza kuendana na utamaduni wetu” alisema.
  • Ni utamaduni upi? Ni wazi City inahitaji kuendelea kuwa timu ya ushindani huku akisaka mafanikio zaidi kwenye soka la Tanzania kabla ya kugeukia kimataifa huku ikiwa na ‘lawi’ ya kuendelea kuwaibua na kuwatumia nyota wa kitanzania walio tele mitaani licha ya vipaji walivyojaliwa.
  • Kwa mashabiki wa City jambo zuri ni kuendelea kusubiri nini kitatokea kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa na maana kubwa alipoitengeneza kesho,huenda jina wanalolitaja litapita na kiu yao kuwa imekatika kama ambavyo ilikatika wakati wanasubiri timu yao kupanda daraja.
  • Lakini kwa sasa sentesi iliyopo kutoka uongozi wa City ni kuwa Kocha msaidizi Meja Mstaafu Abdul Mingange ataendelea kushika usukani wa kuongoza benchi la ufundi la timu ya kizazi kipya nyuma yake akiwa na Mohamed Kijuso na Rashird Kasiga.
  • “Kwa hiyo ni vyema tukaendelea kusubiri nini kitatokea, tunayo maombi mengi lakini kwa sasa hakuna kitakachobadirika kwa maana kuwa Kocha msaidizi Meja Mstaafu Abdul Mingange ataendelea na majukumu ya kuongoza timu sambamba na wasaidizi wake wengine Kijuso na Kasiga mpaka hapo itakapotolewa taarifa nyingine”
  • Hiyo ilikuwa ni kauli ya mwisho ya Katibu Mkuu Kimbe akipigilia msumari kuzima tetesi za kocha mpya wa City, licha ya kukiri kuwa tayari anazo kichwani taarifa za kupigiwa chapuo kwa kocha Phiri na mashabiki wa timu hii.
    Ureno,Ujerumani,ufaransa Ghana,Ivory Coast,Malawi na Afrika Kusini ni baadhi ya nchi ambazo uongozi wa City tayari umepokea barua za maombi kutoka makocha kadhaa wanaomba nafasi ya kuliongoza bechi la ufundi la timu ya kizazi kipya.