Alhamisi, 18 Juni 2015

stars yawasili leo asubuhi Atupele Green, Hassan Isihaka, Hassan Dilunga, Rashid Mandawa na Kelvin Friday waongezwa

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, imewasili leo asubuhi Visiwani Zanzibar tayari kwa maandalizi ya mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya timu ya Uganda kuwania kufuzu kwa CHAN 2016.

Msafara wa Taifa Stars unajumuisha wachezaji 21 na benchi la ufundi 7 ambao wamefikia katika hoteli ya Nungwi Inn, mchezo dhid ya Uganda utachezwa katika uwanja wa Amani kisiwani Zanzibar jumamosi kuanzia majira ya saa 2 usiku.

Stars inakutana na Uganda katika mchezo huo wa awali wa kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Rwanda, kabla ya kurudiana wiki mbili baadae katika uwanja wa Namboole jijini Kampala.

Mara baada ya kurejea kutoka nchini Misri kikosi cha Stars kiliendelea na kambi katika hoteli ya Tansoma na kufanya mazoezi katika uwanja wa Karume kabla ya kuondoka leo asubuhi kuelekea visiwani Zanzibar.

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij amewaongeza wachezaji watano ambao hawakua katika kikosi kilichocheza dhidi ya Misri, kufuatia wachezaji wa kimataifa wa Tanzania kutoruhusiwa kucheza mchezo huo wa CHAN wikiendi hii.

Wachezaji waliongezwa ni Atupele Green, Hassan Isihaka, Hassan Dilunga, Rashid Mandawa na Kelvin Friday, wanaungana na wachezaji Deogratias Munish, Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Salum Mbonde, Aggrey Morris na Nadir Haroub.

Wengine ni Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Mwinyi Haji, Abdi Banda, Frank Domayo, Amri Kiemba, Said Ndemla, Saimon Msuva, na John Bocco.

Aidha Shirikisho la Mpirani wa Miguu barani Afrika (CAF) limetoa mwongozo kuwa mchezaji Mrisho Halfan Ngasa haruhusiwi kucheza CHAN kwa sababu sio mchezaji tena wa ndani, hivyo Ngasa ameondolewa kikosini

Waaamuzi wa mchezo huo wanatarajiwa kuwasili kesho kutoka nchini ambao ni Hudu Munyemana (Rwanda), akisaidiwa na Hakizimana Ambroise (Rwanda), Justin Karangwa (Rwanda), mwamuzi wa akiba ni Issa Kagabo (Rwanda), na kamishina wa mchezo Nicholaus Musonye kutoka Kenya.