Jumapili, 3 Aprili 2016

AZAM FC YASHIKWA SHATI NA TOTO AFRICA YA MWANZA

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Toto African ya Mwanza, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jioni ya leo.
Sare hiyo imeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 51 ikibakia katika nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi mbili na Yanga iliyo nafasi ya pili huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 57, lakini iko mbele kwa michezo miwili dhidi ya wapinzani wake hao.
Mchezo huo uliokuwa wa upinzani kwa pande zote mbili kwa kiasi kikubwa umeharibiwa na mvua kubwa iliyonyesha jijini hapa Mwanza na kufanya uwanja kuloa jambo lililowafanya wachezaji kudondoka chini mara kwa mara na mahesabu ya soka la pasi kushindikana.
Azam FC ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 23 kupitia kwa nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyepiga kichwa kizuri kufuatia krosi safi ya Khamis Mcha ‘Vialli’.
Toto Africans ilijipatia bao lake kupitia kwa Wazir Juma dakika ya 40, ambaye alitumia vema makosa yaliyofanywa na beki Pascal Wawa, aliyeruka juu vibaya kuzuia mpira wa kurusha na kuukosa na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa timu zote kutoshana nguvu.
Licha ya juhudi za Azam FC kutaka kupata mabao kipindi cha pili kwa kuingizwa washambuliaji Allan Wanga,  Didier Kavumbagu  na kiungo Frank Domayo, na kupumzishwa Farid Mussa na Khamis Mcha, jitihada hizo ziligonga mwamba kufuatia Toto Africans kuingia uwanjani kipindi hicho kwa lengo la kupoteza muda.
Pia hali ya uwanja nayo iliharibu mipango yote ya Azam FC ya kutengeneza nafasi. Hata hivyo waamuzi nao walionekana kuvurunda kwenye baadhi ya matukio kwani hata dakika zilizoongezwa tatu walizoongeza zilishindwa kuendana na namna muda ulivyopotezwa na Toto Africans kipindi cha pili.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho saa 2 asubuhi kwa usafiri wa ndege, tayari kabisa kwa kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Ndanda utakaofanyika Jumatano ijayo (Aprili 6) ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi (Dar).