Jumamosi, 5 Machi 2016

NI VITA NA VISASI LEO YANGA NA AZAM TAIFA


KAZI Ipo! Ndio kitakachotokea pale Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, itakapovaana na Yanga katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika  kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo (Jumamosi, Machi 5) saa 10.00 jioni.
Pambano hilo limekuwa likijizolea umaarufu mkubwa kila kukicha kutokana na ushindani unaonyeshwa kwa timu zote mbili na sasa limelizidi kwa mvuto lile la watani wa jadi Simba na Yanga.
Wachezaji wa timu ya Azam FC wana morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huo na kila mmoja amenuia kupambana uwanjani kwa kufanya vizuri ili kutimiza ile adhma waliyojiweka msimu huu ya kuutwaa ubingwa wa ligi.
Tayari benchi la ufundi la Azam FC chini ya Mwingereza Stewart Hall, limeweka wazi kuwa hawana wasiwasi wowote na Yanga kwani wanaijua vilivyo na wapo kamili kwa mapambano ya kusaka pointi tatu muhimu.
“Tumecheza na Yanga mara nne msimu huu kwenye mashindano tofauti, licha ya waamuzi na TFF kuwa upande wao, hawajaweza kutufunga mchezo hata mmoja, uliona kilichotokea kwenye mchezo wetu wa mwisho Yanga alizawadiwa penalti ambayo haikuwa halali.
“Hata katika Kombe la Mapinduzi walipewa bao la kusawazisha ambalo halikuwa halali kwani mpira haukuvuka mstari, tena tulikuwa pungufu ya mtu mmoja baada ya Bocco kupewa kadi nyekundu, licha ya kila mbinu wanazotumia tukicheza nao bado wameshindwa kutufunga tena wakiwa nyumbani mechi zote, hii inaonyesha kuwa wao sio bora,” alisema Kocha Msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica.
Wachezaji wa Azam FC watakaoukosa mchezo huo ni mabeki Racine Diouf, Abdallah Kheri, Aggrey Morris, wanaoendelea na programu ya kurejea uwanjani kufuatia majeraha yanayowasumbua huku Erasto Nyoni naye akikosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja ya ligi baada ya kukusanya kadi tatu za njano, ya mwisho akiipata wiki iliyopita walipotoka suluhu dhidi ya Tanzania Prisons jijini Mbeya.
Kuelekea pambano hilo yafuatazo ni baadhi ya mambo muhimu na takwimu za timu zote mbili kwenye mechi za ligi;
Ubora  
Wakati kila timu ikiwa imecheza mechi 19, kila kitu wameonekana kwenda sawa hasa baada ya kila mmoja kushinda mechi 14, sare nne na kufungwa mmoja na kuzifanya wawe na pointi sawa kileleni mwa msimamo, kila upande ukijikusanyia 46, lakini Yanga ipo juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD).
Ukiachana na hilo mpaka sasa timu hizo ndizo zimefungwa mabao machache kuliko nyingine zote ndani ya ligi, Azam FC ikiwa imeruhusu nyavu zake kuguswa mara 11 na kufunga 34 huku Yanga ikifungwa tisa na kutupia 44.
Nyota wanaozing’arisha
Kwa upande wa Azam FC mabao mengi ya timu hiyo yamefungwa na nyota watatu, Kipre Tchetche anayeongoza kwa kufunga tisa akifuatiwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyeingia wavuni mara nane huku beki wa kulia Shomari Kapombe akitupia saba mpaka sasa.
Kapombe ndio beki pekee wa ligi hiyo mwenye mabao mengi msimu huu, Yanga yenyewe imejipatia mabao mengi kupitia kwa Amissi Tambwe aliyefunga 15, akifuatiwa na Donald Ngoma aliyetupia 11 na Simon Msuva (6).
Rekodi zao
Tokea Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/2009, timu hizo zimekutana mara 15 kwenye ligi hiyo na takwimu zao zote zinalingana kwa kila kitu.
Hii inamaanisha ya kuwa katika mara hizo 15 walizokutana, Azam FC imeshinda mechi tano na kupoteza tano sawa na Yanga, huku zote zikiambulia sare mara tano.
Mara ya mwisho kukutana msimu huu ilikuwa ni kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi, mchezo ulioisha kwa sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likifungwa na Kipre Tchetche na Yanga ikijipatia kupitia kwa Donald Ngoma.
Vita ya ubingwa
Timu yoyote itakayoibuka na ushindi leo itakuwa imepanda kileleni mwa msimamo wa ligi, Azam itakuwa imerejea kwenye kiti hicho cha uongozi na Yanga itakuwa imezidi kujikita kileleni.
Kutokana na idadi ya mechi zao kila mmoja kubakia 10 mara baada ya mchezo wa leo, yoyote atayeshinda leo atakuwa amepiga hatua moja mbele dhidi ya mwenzake katika kuishinda vita ya kutwaa ubingwa msimu huu, lakini haitakuwa kazi rahisi kutimiza hilo katika mechi hizo za mwisho.