Jumatatu, 21 Machi 2016

Msafara wa Kamati ya Bunge Utawala na TAMISEMI Wapata Ajali Mbaya Bagamoyo ....Watu Watano Wafariki Dunia


 
WATU watano wamefariki dunia huku nane wamejeruhiwa, katika ajali iliyoyahusisha magari manne, mawili yakiwa katika msafara wa Kamati ya Bunge Utawala na TAMISEMI maeneo ya Kerege, Bagamoyo Pwani.

Waliofariki katika ajali ni Hilda Msele (59), Mkuu wa Idara ya Mipango ya Uchumi, Makame Ally (40), Dereva wa Tasaf, Khalid Hassan (40), Tunsime Duncan, Mwanasheria wa Wilaya  na Ludovick Palangya, Mchumi.

Majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Taifa ua Muhimbili ni Ibrahim Matovu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bagamoyo, Juliana Msaghaa, Mhandisi wa Maji wilaya, Dorothy Njetile, Mratibu wa Tasaf, George Mashauri, Mweka Hazina wa Wilaya, Amadeus Mbuta, Mshauri wa Tasaf, Julius Mwanganda, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Tauliza Halidi, Mwananchi na Amari Mohamed, Mwananchi.

Aliyepelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na kuruhusiwa ni Grace Mbilinyi ambaye ni Afisa Utumishi na Utawala wa Wilaya.

Ajali hiyo ilihusisha lori la mchanga, gari dogo yaliyokuwa yanatokea Bagamoyo kuja Dar es Salaam, na magari mawili yaliyokuwa kwenye msafara wa Kamati hiyo, yaliyokuwa yanaenda Bagamoyo kwa shughuli zake za kibunge.

Magari yaliyokuwa katika msafara wa kamati hiyo, ni gari la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na gari la Mkurugenzi wa Wilaya ya Bagamoyo ambayo yaligongwa na lori hilo la mchanga na kusababisha vifo vya watu hao na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Ajali hiyo ilitokea baada ya gari dogo lililokuwa linatokea Bagamoyo kupunguza mwendo ghafla na kusababisha lori lililokuwa nyuma yake kuligonga na kuhama upande wa pili na kuyagonga magari mawili yaliyokuwa katika msafara wa kamati ya Bunge.


==