Alhamisi, 11 Februari 2016

Watu 6 Wajeruhiwa Baada Ya Kontena Kuangukia Magari Matatu


Watu sita wamejeruhiwa jana baada ya Lori la Mizigo lenye namba za usalili T 493 DBR lililobeba kontena kuacha njia na kugonga magari matatu kisha kontena kudondoka katikati ya barabara ya Mandela na kusababisha msongamano kwa watumiaji wa njia hiyo.

Tukio hilo lilitokea jana saa 3:00 asubuhi eneo la Tabata Relini wilayani Ilala.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Ernest Matiku alisema watu sita ndiyo walioripotiwa polisi kuwa majeruhi, na wengine ambao idadi yao haifahamiki waliwahi hospitalini wenyewe.

Matiku alisema wanamsaka dereva wa lori hilo ambaye alikimbia baada ya kusababisha ajali hiyo.

Wakisimulia ajali hiyo, mashuhuda walisema kuwa lori hilo lilikuwa kwenye mwendo wa kasi likikimbizana na lori jingine lililobeba kontena.
Lilipofika eneo hilo hilo lenye taa za kuongozea magari, lilijaribu kukwepa daladala lililokuwa kituoni na kuparamia kingo za barabara na baadaye kupinduka.

Baada ya kuparamia na kupinduka, lori hilo lilienda kugonga magari mengine matatu yaliyokuwa katika foleni upande wa pili wa barabara.