Jumanne, 9 Februari 2016

Rais Magufuli Atuma Salamu za Pole Kwa Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Mama Tunu Pinda Aliyepata Ajali ya Gari Jana


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za pole Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Mama Tunu Pinda aliyepatwa na ajali ya gari, iliyotokea jana tarehe 08 Februai, 2016 akiwa safarini kutoka Dodoma kwenda Dar es salaam.

Ajali hiyo imetokea katika eneo la Mkundi lililopo katika Manispaa ya Morogoro ambapo gari aliyokuwa akisafiria Mama Tunu Pinda, ilipinduka baada ya kumgonga mwendesha pikipiki aliyeingia ghafla barabarani.

Katika salamu hizo alizozituma kupitia kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko taarifa za kutokea kwa ajali hiyo na amemuombea Mama Pinda na Majeruhi wengine kupona haraka.

"Kupitia kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu Pinda, naomba unifikishie pole nyingi kwa mkeo Mama Pinda kwa kuumia katika ajali hii, na namuomba Mwenyezi Mungu awaponye majeruhi wote ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku" alisema Rais Magufuli.

Mama Tunu Pinda anaendelea kupata matibabu Jijini Dar es salaam, na hali yake inaendelea vizuri.