Mchezaji Mbwana Samatta aliyejishindia Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa Ndani nchini Nigeria amezawadiwa na serikali kiwanja kilichopo Kigamboni jijini Dar es salaam na fedha taslimu ambazo kiasi chake hakijafahamika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh.Lukuvi anayeonekana katika picha katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Hyyat Regency jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa wa serikali.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria katika hafla hiyo ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Nape Nnauye na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Elisante Ole Gabriel na viongozi wengine wengi wa serikali na wanamichezo.
Mbwana Samatta aliyekuwa akicheza mpira wa kulipwa katika timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inayomilikiwa na tajiri wa madini na aliyewahi kuwa Gavana wa jimbo la Katanga nchini humo Moise Katumbi anatarajiwa kujiunga na timu ya KRC Genki ya Belgium barani ulaya.