Hatimaye
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, jana
ameonekana hadharani katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya
Mapinduzi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Jecha
ambaye inaaminika alikuwa mafichoni tangu alipotangaza kufuta matokeo
ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, alionekana ameketi
kwenye jukwaa kuu la viongozi, jirani na Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, Jaji Francis Mutungi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John
Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Kuonekana
kwa Jecha hadharani kumezua mijadala mitaani na hata katika mitandao ya
kijamii, huku wengi wakihoji alikuwa wapi mara baada ya kufuta matokeo
ya uchaguzi.
Watu
mbalimbali wamekuwa wakihoji kuonekana kwa Jecha hadharani jana, siku
ambayo Dk. Shein alitumia maadhimisho ya Mapinduzi kutangaza kwamba
uchaguzi wa marudio Zanzibar iwe isiwe utafanyika.
Oktoba
28, mwaka jana majira ya saa sita mchana kwenye Ofisi za Tume ya
Uchaguzi Zanzibar zilizopo Kilimani mjini Unguja, ilikuwa ndiyo siku ya
mwisho kuonekana Jecha hadharani.
Siku
hiyo huku akiwa chini ya ulinzi wa vijana wawili wanaoaminika kuwa ni
makomandoo wa Jeshi la Ulinzi wa Tanzania (JWTZ) waliovaa kiraia, Jecha
alitangaza kuufuta uchaguzi wa Zanzibar mbele ya vyombo vichache vya
habari.
Alitumia
dakika mbili tu kuvitangazia vyombo hivyo vya habari juu ya adhima yake
ya kuufuta uchaguzi na kutoa sababu zilizomfanya kufanya hivyo ikiwamo
kuharibiwa kwa uchaguzi kisiwani Pemba.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kutoa taarifa yake kwa vyombo hivyo, Jecha hakutaka kuulizwa maswali.
Oktoba
27, mwaka jana ikiwa ni siku moja kabla ya kutangaza kufuta matokeo ya
uchaguzi, Jecha pia hakuonekana kwenye kituo cha kutangaza matokeo
kilichokuwa katika Hoteli ya Bwawani kwa kile kilichodaiwa alipata
matatizo ya kiafya na hivyo kumwachia kazi hiyo Makamu Mwenyekiti wa
ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa.
Siku
hiyo majira ya saa kumi jioni, askari wa JWTZ walizingira kituo cha
Bwawani na kuwaamuru watu waliokuwa ndani kutotoka nje na hata wale
walioko nje ya kituo hicho kutosogea.
Watu
waliokuwa ndani ya kituo hicho wengi wao walikuwa waandishi wa habari
wa vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi pamoja na baadhi ya
wawakilishi wa vyama vya siasa waliofika kusikiliza matokeo ya uchaguzi.
Kutokana
na kile kinachoonekana kuendelea kupasuka kwa hali ya kisiasa visiwani
Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein, amesisitiza uchaguzi utarudiwa baada ya awali matokeo
yake kufutwa na ZEC.
Akihutubia
katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika Uwanja wa Amaan jana, Dk. Shein alisema uchaguzi huo utarudiwa
kwa mujibu wa katiba na sheria.
“Kila
mmoja anajua kilichotokea katika uchaguzi Zanzibar baada ya Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi kutokana na kasoro
zilizogundulika kutokea wakati wa uchaguzi huo,” alisema Dk. Shein na kuongeza:
“Suala
la kurudiwa kwa uchaguzi liko palepale na utarudiwa kwa mujibu wa
katiba na sheria, hivyo nawaomba wananchi muwe na uvumilivu na upendo
wakati tukisubiri kutangazwa kwa tarehe ya kurudiwa uchaguzi.”
Licha
ya kwamba kila upande umeshaweka msimamo wake, lakini Dk. Shein alisema
mazungumzo ya kusaka suluhu yanaendelea baina ya pande hizo na kwamba
taarifa ya mazungumzo hayo itatolewa punde yatakapokamilika.
“Tangu
kutokea kwa mgogoro huu tulishauriana kukutana viongozi sita waliopo
madarakani na waliostaafu ili kufanya mazungumzo ya kusaka suluhu na
taarifa itatolewa pindi mazungumzo yatakapokamilika,” alisema Dk. Shein.