Rais John Magufuli amelaani vikali kitendo cha Wabunge wa Vyama vya Upinzani kuzomea leo bungeni.
Rais Magufuli ameeleza kuwa tabia iliyofanywa na wabunge hao inaonesha jinsi ambavyo hawajakomaa kisiasa na kuwaita watoto huku akimpongeza Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kwa kuendelea kubaki Bungeni.
“Ndio maana nimempongeza sana Mheshimiwa Zitto. Mheshimiwa zitto umekomaa na naamini hata wana CCM kule Kigoma walikuchagua,”alisema rais Magufuli.
“Mmeona tuna kazi kubwa, bado tuna watoto wengi. Tuendelee kuwavumilia, nadhani na watanzania wameona,” aliongeza.
Aliwataka wabunge wote kusimama pamoja bila kujali itikadi zao za vyama na kuwasisitiza kuwa wanapaswa kuhakikisha kuwa Bunge la 11 linakuwa bunge la kihistoria na kuacha masuala ya kupigana vijembe, kuzomeana na kutoka nje.
Kwa upande wake Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai alimuomba radhi rais Magufuli na Shein kwa kile kilichoanywa na wabunge wa Ukawa huku akiahidi kuwa hali hiyo haitajirudia tena.
Ndugai aliwaonya wabunge kuwa kitendo kilichofanywa ni cha aibu hivyo hatawavumilia tena na kwamba wabunge wanaweza kumfanya akawa Spika mpole ama kumfanya awe Spika ‘mbabe’.
“Mnaweza kunifanya nikawa Spika mbabe sana… leo iwe mwisho. Ni kwa sababu wazee hawa walikuwepo. Lakini wazee hao wasipokuwepo, wakifanya tena tabia hii, basi… nisiseme sana,” alisema.