Mshambuliaji mahiri wa Mbeya City Fc Themi Felix ‘Mnyama’ ameongeza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kukipiga ndani ya kikosi cha Juma Mwambusi.
Akizungumza mara baada ya kuongeza kandarasi yake juzi usiku kwenye ofisi za timu zilizopo jengo la Mkapa Hall hapa jijini Mbeya mshambuliaji huyo aliyefanikiwa kupachika wavuni mabao 5 kwenye ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliomalizika alisema bado anafuraha kuwa sehemu ya kikosi cha City.
“Baada ya ligi kumalizika, nilipata ofa nyingi kutoka timu kadhaa ikiwemo timu yangu ya zamani,binafsi nina amani kubwa kuwa sehemu ya kikosi cha City,msimu uliopita nilifanikiwa kufunga mabao 5, nina furaha na hii ndiyo sababu yangu kuamua kubaki kwenye timu hii” alisema.
Akiendelea zaidi Themi alisema kuwa ushirikino mzuri alioupata kutoka kwa viongozi, mashabiki na wadau wa City katika msimu uliopita umemfanya kuwa na furaha kubwa tofauti na mahala alipokuwa awali.
“Ni jambo zuri na lenye furaha unapocheza kwenye timu ambayo unapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi,mashabiki na wadau wengine, nimekuwa na amani hapa kuliko nilipokuwa awali, City ina mipango mizuri naamini tutakuwa na mafanikio siku za usoni” alisema.
Katika hatua nyingine Themi amesema kuwa kuondoka kwa nyota waliokuwa wanacheza chini ya kocha Juma Mwabusi msimu uliopita ni jambo la kawaida ambalo haliwezi kuiyumbisha City kwa sababu tayari ina kikosi kikubwa ambacho kinaweza kupambana na kupata matokeo mazuri.
“City bado ina kikosi kikubwa, U20 kuna vijana wengi wenye vipaji na wenye uwezo wa kupambana, wakati Rafael Daud anapandishwa hakuna aliyesadiki, lakini leo ni mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi, binafsi naamini kuondoka kwa akina Kaseke na wenzake hakutaiteteresha timu” alimaliza.