Jumatano, 6 Mei 2015

JUVE WASHINDA, TEVEZ APIGA TUTA LA USHINDI DHIDI MABINGWA REAL


Mabingwa wa Italy, Juventus, wakiwa kwao Juventus Arena Jijini Turin Nchini Italy, wameanza vyema Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONZ LIGI walipowafunga Mabingwa Watetezi Real Madrid Bao 2-1.
Juventus walipata Bao lao la kwanza Dakika ya 8 kutokana na pasi safi ya Marchisio kumkuta Carlos Tevez ambae Shuti lake lilitemwa na Kipa wa Real Casillas na kumkuta Alvaro Morata aliekwamisha Mpira wavuni.
Real walisawazisha Dakika ya 27 kwa Bao la Kichwa la Ronaldo kufuatia krosi ya James Rodriguez.
Hadi Haftaimu Magoli yalikuwa 1-1.
Kipindi cha Pili, Juve walifunga Goli la Pili baada ya kuokoa Kona ya Real na kuanza kaunta ataki kupitia Morata ambae alimpenyezea Tevez alieangushwa na Carvajal na Refa wa England Martin Atkinson kutoa Penati.
Tevez alifunga Penati hiyo na Juve kutangulia 2-1.
Baada Juve kwenda 2-1 mbele wakabadilisha Mfumo na kuanza kutumia 5-3-2 walipomtoa Sturaro na kumwingiza Barzagli ili kuweka ngome ya Masentahafu Watatu ili kutetea uongozi wao kwa kujihami zaidi na kuvizia mashambulizi ya kushtukiza.
Timu hizi zitarudiana tena Mei 13 huko Jijini Madrid Uwanjani Santiago Bernabeu.