Baada ya michezo minne ugenini kikosi cha Mbeya City Fc kinarejea
kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya jumapili hii kuivaa Yanga ya Dar
es Salaam katika mfululizo wa kindumbwendumbwe cha ligi kuu ya soka
Tanzania Bara huu ukiwa ni mchezo wa ‘kiporo’ baada ya kuahirishwa
awali kufuatia uwepo wa michuano ya kombe la Mapinduzi.
Akizungumza kuelekea mchezo huu Kocha wa City Juma Mwambusi amesema
kuwa anafahamu uzito wa mechi hiyo hasa ukizingatia matokeo
yaliyokuwepo msimu uliopita baina ya timu hizo hivyo kwa namna yoyote
mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa City itacheza ikiwa na shauku ya kulipa
kisasi cha kupoteza mchezo wa mzunguko wa pili msimu uliopita.
“Huu utakuwa ni moja ya michezo migumu tutaingia uwanjani tukiwa na
kumbukumbu ya kupoteza mchezo wetu wa pili dhidi yao msimu uliopita,
tulianza ligi vibaya msimu huu hasa katika michezo saba ya mwanzo,
mara hii tuko vizuri ndiyo maana tuliweza kuifunga Simba nyumbani,najua
utakuwa mchezo mgumu lakini matokeo ndiyo kitu pekee tunachokihitaji
hivi sasa” alisema MWAMBUSI