Jumapili, 13 Desemba 2015

Wafanyabiashara 15 Waliokaidi Agizo la Rais Kukiona Cha Moto


MAKAMPUNI 15 yaliyokwepa kodi baada ya kutorosha makontena yao, yamejisalimisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini yameshindwa kulipa kodi ndani ya siku saba za msamaha wa Rais John Magufuli.

Kodi inayodaiwa kwa kampuni hizo ni Sh bilioni 3.75, hivyo watachukuliwa hatua za kisheria kwa kukwepa kulipa kodi, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango alisema hayo jana wakati akielezea makusanyo ya kodi ya makontena yaliyoondolewa katika bandari kavu ya Azam, kinyume cha sheria pamoja na kumalizika kwa siku saba alizotoa Rais Magufuli kwa wafanyabiashara hao kulipa kodi waliyokwepa, bila kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.

Dk Mpango alisema siku hizo saba zimefikia kikomo juzi, hivyo hatua kali za kisheria kwa wafanyabiashara ambao hawakulipa kodi katika kipindi hicho zinafuata hivyo wasubiri cha moto.

“Tumewasihi waje kulipa kwani huruma ya Rais sasa imeisha... tulifanya uhakiki na kuthibitisha kuwa kampuni hizo zipo. Wamekuja kulalamika lakini hakika hakuna atakayesamehewa kulipa na sasa tunafuata mkondo wa sheria ili kuwafikisha mahakamani,” alisisitiza.

Wadaiwa 
Alitaja kampuni hizo kuwa ni Ahmed Saleh Tawred anayedaiwa Sh milioni 59.23; Cla Tokyo Limited Sh milioni 77.52; Farida Abdullah Salem Sh milioni 75.33 na Juma Kassem Abdul Sh milioni 190.18.

Wengine ni Libas Fashion Sh milioni 52.94; Rushy Wheel Tyre Center Co Ltd, Sh bilioni 1.8; Said Ahmad Hamdan Sh milioni 68.36; Said Ahmed Said Sh milioni 68.73 na Salum Continental Co Ltd Sh milioni 151.17.
 Pia yumo Salum Link Tyres Sh milioni 343.44; Simbo Yonah Kimaro, Sh milioni 69.22; Snow Leopard Building Material Co Ltd Sh milioni 93.97; Swaleh Mohamed Swaleh Sh milioni 34.68; Tybat Trading Co Limited, Sh milioni 598.69 na Nasir Saleh Mazrui Sh milioni 70.10.

Alisema mpaka kufikia jana TRA walikuwa wamekusanya Sh bilioni 10,643.004,948.46 kutoka kwa kampuni 28 ambapo kampuni 13 zimelipa kodi yote iliyokadiriwa, ambayo ni Sh 4,167,130,173.89 na Sh 2,303,637,554.57 kutoka kampuni 15 zilizolipa sehemu ya kodi iliyokadiriwa.

Dk Mpango alisema Sh bilioni 4.17 zimelipwa na kampuni ya Azam ICD, ikiwa ni dhamana ya kodi iliyokwepwa, hivyo atatakiwa kumaliza kulipa kodi yote inayodaiwa kwa mujibu wa nafasi yake kama mwenye dhamana.

Alisema wakati utekelezaji huo ukiendelea, ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo ya makontena yaliyoondolewa bandarini kinyume cha sheria na taratibu za forodha, TRA imefungua akaunti maalumu katika Benki Kuu yenye namba 9921169785 inayoitwa Commissioner for Customs and Excise – Container Account.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, mpaka sasa watumishi 36 wa TRA wanaotuhumiwa kushiriki katika upotevu wa kodi kutokana na makontena hayo kuondoshwa bandarini.

Watumishi wachongewa 
Aidha, alisema TRA imepata taarifa zisizopungua 15 kutoka kwa wananchi kuhusu mali za kifisadi na mwenendo mbaya wa baadhi ya watumishi na walipakodi wanaokwepa kodi. 
Aliwashukuru wananchi waliotoa taarifa na kuwaomba wengine wajitokeze kutoa taarifa zaidi na mamlaka hiyo inawahakikishia kuwa itawalinda.

Dk Mpango alisema wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais katika ukusanyaji wa mapato, ikiwa ni pamoja na kupiga picha makontena yote badala ya sampuli ya kontena ilivyo sasa na wanafanya utaratibu wa kupata mashine za kupiga picha za nyongeza.