Pamoja na kucheza vizuri muda wote wa kipindi cha pili,Mbeya City Fc imejikuta ikilazimishwa sare ya kufungana bao 2-2 na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Katika mchezo huo uliokuwa wa kusisimua muda wote, Mtibwa Sugar walikuwa wa Kwanza kupata bao mapema dakika ya 6 lililofungwa na Ally Sharifu kufuatia makosa ya walinzi wa City kumuacha mfungaji wakidhani ameotea.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaongeza nguvu vijana hao wa Meky Mexime kuendelea kulishambulia lango la City na kuanikiwa kupata bao lingine mara hii likifungwa na Said Bahanuzi kwa mkwaju wa penalti baada ya Yusuf Abdalah kuunawa mpira akiwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Said Kayombo kuamuru kupigwa kwa penalti hiyo.
Baada ya kufungwa bao la pili vijana wa City walilazimika kubadili mfumo na kuanza kutumia pasi fupi fupi wakipanga mashambulizi kutoka katikati ya uwanja eneo lililouwa likimilikiwa vyema na Rafael Daud na Kenny Ally na kufanikiwa kupata bao la kwanza kupitia Haruna Moshi ‘Boban’ aliyefunga kwa kichwa cha ‘kuchumpa’ akiunganisha krosi ya Hassan Mwasapili na kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 2-1.
Kipindi cha pili kocha Abdul Mingange alifanya mabadiliko kwa kumtoa Geoffrey Mlawa na nafasi yake kuchukuliwa na Issa Nelson, pia akamtoa Rafael Daud na kumuingiza Hamad Kibopile, mabadiliko ambayo yaliisaidia City kupata bao la kusawazisha kupitia Issa Nelson aliyefunga kwa kichwa kufuatia krosi safi ya Haruna Moshi.
City iliendelea kulishambulia lango la Mtibwa ikisaka bao la ushindi, zikiwa zimebaki dakika 5 mpira kumalizika Joseph Mahundi nusura aipatie timu yake bao la 3 baada ya kuiwahi pasi ya Temi Felix na kupiga shuti kali ambalo lilishindwa kulenga lango la Mtibwa na mpira kutoka nje,hivyo hadi dakika 90 zinakamilika matokeo yalibaki sare ya bao 2-2.
Mara baada ya mchezo kocha Mingange alisema kuwa vijana wake walikosa bahati licha kucheza vizuri kipindi chote cha pili huku akisifu kazi nzuri ya Issa Nelson aliyeingia kipindi cha pili na kusawazisha bao.