EDWARD Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu leo saa 5 asubuhi atachukua fomu kugombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Hatua ya Lowassa kuchukua fomu ya urais inakuja siku mbili chama hicho katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam ambamo aliahidi kuiongezea Chadema nguvu ya wanachama kuelekea ushindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu kuiondoa CCM madarakani.
Taarifa ya Lowassa kuchukua fomu hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Makao Makuu ya Chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“leo saa 5 asubuhi hapa makao makuu ya chama, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa atachukua fomu ya kugombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema. Kutakuwa na shamrashara nyingi sana. Na kutakuwa na matokeo mengi baada ya leo,” amesema Mwalimu.
Aidha, Mwalimu ametoa ufafanuzi kuhusu uwepo wa minong’ono kwamba Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Tundu Lissu, Mwanasheria wa chama hicho kwamba walisusia tukio la Lowassa kujiunga na Chadema.
“Juzi ilipita minong’ono mingi tu, katibu mkuu wetu yupo kwenye majukumu mengi. Katika kipindi hiki cha uchaguzi tuna mambo mengi. Hatuwezi wote kuwa pamoja. Tunagawanyika kulingana na programu tulizonazo,” amefafanua Mwalimu.