RAIS TFF AAGIZA USIMAMIZI MECHI ZA MWISHO VPL
Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewaagiza
wasimamizi wa vituo vya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuhakikisha sheria na
taratibu zote za mechi zinafuatwa.
Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) msimu huu 2014/2015 inafikia tamati kesho (Mei 9, 2015)
ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani katika mechi ambazo ndizo
zitakazotoa hatma ya timu zinazoshuka daraja.
Mechi hizo
zitakuwa kati ya Ndanda na Yanga (Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara),
JKT Ruvu na Simba (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Azam na Mgambo
Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Stand United na Ruvu Shooting
(Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), Kagera Sugar na Tanzania Prisons
(Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mbeya City na Polisi Morogoro (Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Mtibwa Sugar na Coastal Union
(Uwanja wa Manungu, Morogoro).
JERRY MURO APIGWA FAINI MILIONI 5
Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF iliyoketi jumanne
tarehe 5 Mei, 2015 imempiga faini ya sh. 5,000,00 (milioni tano), Afisa
Habari wa klabu ya Yanga SC Jerry Muro kwa kutoa kauli za chuki,
kisirani na uchochezi dhidi ya uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) nchini na
TFF.
Akitoa utetezi
wake mbele ya Kamati ya Nidhamu, Jerry Muro alikiri na kujutia kufanya
kosa hilo na kudai ilitokana na ugeni wake katika uongozi wa michezo,
kwa kuzingatia hilo kamati ilimuepusha na adhabu ya kufungiwa..
Kwa mujibu wa
Ibara ya 53 (2)ya Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la 2012, kwa
kuidhalilisha TFF na Bodi yake ya Ligi mbele ya umma, kamati imemtoza
faini ya sh. 5,000,000 (millioni tano), Jerry Muro na kuwaonya viongozi
wengine wa familia ya mpira wa miguu kutojihusisha na vitendo vya
matamshi ya aina hiyo.
Shitaka
linalomhusisha mchezaji wa Yanga, Amissi Tambwe kumshika kwa
kumdhalilisha mchezaji wa Simba SC Juuko Mursheed, na kiongozi wa Friend
Rangers Hery Chibakasa wa Friends Rangers kuhamasisha vurugu katika
mchezo wa timu yake na dhidi ya Majimaji ya Songea Januari 29, 2015,
kamati imeahirisha mashitaka hayo mpaka tarehe nyingine itakapopangwa.
Kamati
iliahirisha malalamiko dhidi ya Mohamed Hussein, Muhibu Kanu, Manfred
Luambano, Venance Joseph, Mussa Senyange, Saleh Ali, Shafii Maganga na
Ismail Salim baada ya kupokea taarifa za udhuru zilizosbabishwa na mgomo
wa madereva wa mabasi ya abiria ya mikoani.
KUMRADHI WANAHABARI
Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Mwesigwa Selestine ameomba
radhi kwa vyombo kufuatia madai ya waandishi wa habari kupata usumbufu
wakati wa utoaji wa Zawadi kwa Mabingwa na washindi wa pili wa Ligi Kuu
ya Vodacom.
Mwesigwa
alisema kwa niaba ya TFF anaomba radhi kwa usumbufu wowote uliowapata
waandishi na wadau wote walioshindwa kushuhudia vema tukio hilo.
“TFF na FIFA
vinatambua umuhimu na nafasi ya wanahabri na vyombo vya habari si tu
katika kuutangaza mchezo, bali pia katika kutia chachu maendeleo ya
mchezo wenyewe “ alisema Mwesigwa.
Hali mbaya ya
hewa ilivuruga utaratibu uliokuwa umepangwa awali kuanzia itifaki ya
shughuli za kabla na wakati wa mchezo na zile za utoaji tuzo.
Aidha Mwesigwa
alisema TFF itaendelea kushirikiana vema na jumuiya ya wanahabari ikiwa
ni pamoja na kuhakikisha kwamba wana mazingira mazuri wanapofanya kazi
kwenye matukio ya mpira wa miguu.