MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga SC jioni ya leo wamelazimishwa sare ya bila kufungana na SC Villa ya Uganda katika mchezo wa kirafiki, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga SC watajilaumu wenyewe kwa sare hiyo, kwani walipata nafasi kadhaa za kufunga ikiwemo penalti, iliyopaishwa na mchezaji bora wa Ligi Kuu, Simon Msuva dakika za lala salama.
Timu hizo zilianza kushambuliana kwa zamu, huku zote zikicheza soka maridadi ya utulivu na pasi za uhakika kabla ya dakika ya 27 Kasumba Omary wa Villa nusura kumzunguka Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ lakini beki wa kulia Oscar Joshua akaondosha mpira kwenye hatari.
Dakika ya 28 Achema Robert alipiga shuti kali likatoka nje, kabla ya shuti lake lingine kudakwa na kipa wa Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ dakika ya 33.
Malimi Busungu wa Yanga SC alipiga nje dakika ya 32 kufuatia pasi nzuri ya Amisi Tambwe. Busungu tena dakika ya 35 alimdakisha kipa wa Villa, Sebwato Nicolaus baada ya kupiga ndani ya boksi.
Tambwe naye alipoteza nafasi ya kufunga dakika ya 34 baada ya shuti lake kudakwa na kipa wa Villa, Sebweto.
Katika mchezo huo, Kocha mpya wa Simba Dylan Kerr aliingia kuwatazama wapinzani, kipindi cha pili Yanga SC walitengeneza nafasi nzuri, lakini wakashindwa kutumia.
Dakika ya 50 Deus Kaseke aligongesha mwamba, dakika ya 54 krosi nzuri ya Juma Abdul ilidakwa na kipa wa Villa, Sebwato.
Yanga SC ilipata pigo dakika ya 71, baada ya Nahodha wake, Cannavaro kuumia juu ya jicho na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Pato Ngonyani aliyekwenda kucheza vizuri.
Winga mpya machachari wa Yanga SC, Godfrey Mwashiuya aliunganisha vizuri krosi ya Kpah Sherman dakika ya 76, lakini beki wa Villa, Wasibi akaokoa mpira ukiwa unaelekea nyavuni.
Msuva akapaisha penalti dakika ya 78 baada ya kipa wa Villa kumuangusha Kaseke kwenye eneo la hatari na dakika ya 80 Mwashiuya aliipiga shuti maridadi lilodakwa na kipa wa villa .