Jumapili, 12 Juni 2016

CHADEMA, CCM Watofautiana Kuhusu Naibu Spika, Dk Tulia Ackson


Wakati Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Mbeya ikiutaka uongozi wa Bunge kuwachukulia hatua kali wabunge wa upinzani wanaosusia vikao vya Bunge, Chadema, Kanda ya Magharibi, imemtaka Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kujitafakari upya kama anafaa kuendelea na nafasi hiyo.


Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM na Chadema walitoa kauli hizo ikiwa ni siku ya 12 tangu wabunge wa upinzani kususia vikao vinavyoendesha na Dk Tulia.


CCM walisema kitendo kinachofanywa na Chadema kinachochea siasa za kibaguzi badala ya kufanya kazi ya kutunga sheria ya kusimamia Serikali kwa maslahi ya wananchi.


Katibu wa Siasa Itikadi na uenezi Mkoa wa Mbeya, Bashuru Madodi aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa kitendo kinachofanywa ni kinyume cha maadili na mwongozo wa nchi na kumpongeza Dk Tulia kwa msimamo wake wa kuliongoza Bunge bila kujali ubabaishaji wa wabunge wa upinzani.


“Kitendo cha wabunge kutoka nje wakati wa vikao na kupiga soga ni utovu wa nidhamu na kutoheshimu kiti cha spika na hivyo wajiulize bungeni walikwenda kwa maslahi ya wananchi au la? ”alihoji.


Madodi alisema pia halmashauri kuu inalaani vikali matamko yanayotolewa ya wabunge wa upinzani ya kuzunguka nchi nzima kufanya siasa za kuwahadaa wananchi kuwa wameonewa bila kutambua kuwa wao ni chanzo cha uvunjifu wa amani kwa kutozingatia na kufuata kanuni na taratibu za Bunge.


Kadhalika alisema ni vyema Bunge kufanya maamuzi ya kutowalipa posho wabunge watakaokuwa wakishindwa kuhudhuria vikao vyake.


“Uongozi wa Bunge usitetereke kwa vitendo vya ubabaishaji wa vyama vya upinzani na uendelee kuchukua hatua stahiki dhidi ya wabunge wanaoendelea na vitendo vya utovu wa nidhamu badala ya kuwasilisha kero za wananchi waliowachagua,” alisema.


Kaimu Katibu CCM Mkoa wa Mbeya, Lobe Zongo alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kurejesha nidhamu ya utendaji wa kazi serikalini hali itakayosaidia uchumi wa nchi kusonga mbele na kurejesha nidhamu.


 “Haya yote ni matunda ya Rais wa awamu ya tano kwa kweli anastahili pongezi kwa uwajibikaji na utendaji wa kazi kwa watendaji ndani ya chama na serikalini,”alisema.


Katibu wa Chadema Kanda ya Magharibi, General Kaduma alimlaumu Tulia akidai hana uchungu na wananchi kwa kuwa hakuchaguliwa kwa kupigiwa kura kama walivyokuwa manaibu waliomtangulia.


 Kaduma alidai Naibu spika huyo amevunja kanuni za Bunge na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani kwa kushiriki kuondoa vipengele muhimu katika hotuba ya waziri kivuli wa mambo ya ndani, Godbles Lema.


Katibu huyo ambaye amechukua nafasi ya aliyekuwa Katibu wa Chadema Kanda hiyo, Christopher Nyamwanji, aliitaka Serikali kuingilia kati uamuzi uliotolewa na Kamati ya Maadili ya Bunge akidai hayakuwa sahihi.


“Mchango wa wabunge waliozuiliwa kuingia bungeni ni mkubwa katika Bunge hili la bajeti ila utakosekana kutokana na uamuzi uliochukuliwa na naibu spika ambao kimsingi unaminya demokrasia nchini,” alidai.


Pia, alikemea kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia mikutano na kutumia silaha za moto kutawanya umma akisema kinasababisha uvunjifu wa amani.


Amelitaka jeshi hilo kuacha kufanya kazi kwa maslahi ya CCM na badala yake wawe walinzi wa amani nchini kwa kufanya kazi bila upendeleo.


Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Tabora, Francis Msuka alisema wajibu wa kufanya mikutano ya siasa nchini ni wa muda wote kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana.


Alisema kumekuwa na matukio ya viongozi wa Chadema kunyanyaswa na Jeshi la Polisi huku viongozi wake ngazi ya vijiji wakifanyiwa mizengwe ili wasitimize majukumu yao kikamilifu.